Dar es Salaam. Wakati wowote Rais Jakaya
Kikwete anatarajia kuipanga safu mpya ya Baraza la Mawaziri kwa kuteua
waziri mwingine wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi baada ya
kumwondoa aliyekuwepo, Profesa Anna Tibaijuka.
Mara nyingi katika uteuzi wake Rais Kikwete
amekuwa na utaratibu wa kuwapandisha baadhi ya naibu mawaziri kuwa
mawaziri, kuwapa uwaziri wabunge ambao amewateua au kuteua waziri kutoka
katika mkoa ambao anatokea waziri aliyeondolewa.
Profesa Tibaijuka ambaye ni Mbunge wa Muleba
Kusini mkoani Kagera anakuwa waziri wa tatu kutoka mkoa wa Kagera
kuondolewa madarakani katika uwatala wa Rais Kikwete. Ameondolewa
kutokana na kukabiliwa na kashfa ya uchotaji wa fedha katika Akaunti ya
Tegeta Escrow.
Wengine walioondolewa kutoka mkoa huo ni aliyekuwa
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kutokana na
kushindwa kuwajibika katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili
pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi
aliyeondolewa kutokana na sakata la Richmond.
Iwapo Rais Kikwete atazingatia utaratibu wake wa
kuteua waziri kutoka mkoa ambao waziri aliyeondoka anatoka, huenda
nafasi iliyoachwa wazi na Profesa Tibaijuka kuchukuliwa na Charles
Mwijage (Muleba Kaskazini), Gosbert Blandes (Karagwe).
Assumpter Mshama (Nkenge), Jasson Rweikiza (Bukoba
Vijijini), Eustace Katagira (Kyelwa), Deogratius Ntukamazina (Ngara) na
Dk Antony Mbasa (Biharamulo Magharibi).
Kama akitumia utaratibu wa kumpandisha naibu
mawaziri, huenda nafasi hiyo ikachukuliwa na Naibu Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene ambaye ni Mbunge wa
Kibakwe au naibu mawaziri kutoka wizara nyingine kama alivyowahi kufanya
mara nyingi.
Kwa mujibu wa Ibara ya 66 (1) (e) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ilivyofanyiwa
marekebisho inampa mamlaka Rais kuwateua wabunge 10, mpaka sasa
ameshawateua wanane na kubakiza nafasi mbili pekee.
Kati ya wabunge wanane walioteuliwa na Rais Kikwete, watano walipewa wizara za kuziongoza.
Wabunge hao na wizara zao kwenye mabano ni Shamsi
Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Profesa Makame
Mbarawa (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia).
Wengine ni Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na
Madini), na Saada Mkuya (Nishati na Madini) na Janet Mbene (Naibu Waziri
Viwanda na Biashara) na Dk Asha-Rose Migiro.
Dk Migiro aliteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na
Sheria. Wabunge ambao wameteuliwa na Rais, lakini hakuwapa uwaziri
mpaka sasa ni Zakia Meghji na James Mbatia- Mwananchi
إرسال تعليق