Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika inayoendelea nchini
Guinea ya Ikweta inazidi kupamba moto. Kama kawaida yetu, Tanzania
tumeendelea kuwa watazamaji.
Mara ya mwisho Tanzania ilikuwa kwenye michuano
hiyo mwaka 1980, ilipofanyika nchini Nigeria. Tangu wakati huo,
hatujawahi tena kushiriki fainali hizo.Kwa mashabiki wa soka
wanaofuatilia fainali hizo, watakubali kuwa safari yetu ya kucheza
fainali hizo kwa mara nyingine ni ndefu na inayohitaji maandalizi ya
muda mrefu.
Kwa namna soka letu lilivyotawaliwa na mambo mengi
ya nje kuliko uwanjani, ni rahisi kushawishika kuamini kuwa tuna safari
ndefu kabla ya kufikia mafanikio.
Mafanikio ya mchezo wa soka siyo sawa na bahati ya
mtu kulala maskini na kuamka tajiri. Hakuna njia ya mkato kufanikiwa
katika soka kama wengi wanavyoweza kufikiria.
Tunaendelea kuwa watumwa wa kushindwa kukubali
ukweli kwamba, safari yetu ya kurejea mbio za mwaka 1980, hazihitaji
longolongo na porojo za kujifurahisha kutoka kwa viongozi wetu.
Ushindani unaoonekana kwenye mashindano hayo,
unatufanya tuamini kuwa bila juhudi na kujituma, tunaendelea kuwa
mashuhuda wa fainali hizi kupitia televisheni kila siku.
Leo hii viongozi wetu wamebaki kupiga kelele za
ukata kila kukicha. Inasikitisha kiongozi anakosa ubunifu wa kutafuta
njia za kuhakikisha michezo inasonga mbele, badala yake analia
njaa.Viongozi wanasahau kuwa wana dhamana yao ya kuongoza ni pamoja na
kuwa wabunifu katika kuhakikisha mafanikio yanapatikana. Kwa viongozi
wetu hilo hawana.
Katika hali kama hiyo unategemea lini Taifa
litasonga mbele? Viongozi wamebweteka ofisini, hawaendi viwanjani na
kujifunza mambo yanayotokea huko.
Soka letu limejaa fitina nyingi, kuanzia ndani ya
uwanja hadi nje. Kila kitu tunakichukulia kwa uzito mwepesi, maswali
magumu tunayaandalia majibu mepesi, halafu tunataka kwenda Fainali za
Kombe Mataifa ya Afrika.
Hivi tunadhani ni lini tutakwenda kufanikiwa kama
wale ambao walipaswa kuwa mfano mzuri wanafanya mambo kinyume chake? Leo
hii mwamuzi wa soka kuchezesha mechi analazimika kujishauri zaidi ya
mara mbili kwa hofu ya kupigwa na wachezaji kwa madai ya upendeleo.
Hatuna sababu ya kupata shida kuamini kuwa,
wachezaji wanaofanya hivyo wanaandaa Taifa la vijana wa fujo viwanjani.
Tunawajengaa nidhamu mbaya, kwamba kama mwamuzi amekosea basi adhabu
yake ni kupigwa.
Ni badiliko tu ndiyo yatakayokomboa soka la Tanzania

إرسال تعليق