Hali gani mpenzi msomaji wa makala haya, ni matumaini yangu kwamba uko salama kabisa. Karibu kwenye ukurasa wetu huu mzuri, tujadili na kubadilishana mawazo kuhusu mambo yanayohusu ujasiriamali.
Leo ningependa kujadiliana na wewe msomaji wangu kuhusu vitu ambavyo kama usipovizingatia, vinaweza kusababisha ushindwe kufikia mafanikio ya kweli kwa mwaka 2015 kama ifuatavyo.
1. MATUMIZI YA HOVYO YA PESA
Wajasiriamali wengi, wakishaanza tu kupata mafanikio huwa wanadanganyika kwa kuona pesa nyingi zinaingia kwenye msimu fulani wa mwaka na kujikuta wakizitumia kwa fujo bila kujua kuwa kuna matumizi mengi muhimu kama kulipa mishahara, kulipa kodi na mambo mengine mengi.
Baadaye hushangaa tu hakuna pesa za kuendeshea biashara (working capital). Ni hapo ndipo utasikia kauli kama vile ‘mtaji umekata’! Hii ni kwa sababu ya matumizi ya hovyo ya pesa.
2. KUFANYA BIASHARA NA WATU WASIOFAA
Wengi wameumizwa kwa kuchagua mshirika mbaya mwanzoni. Wakati mshirika mmoja yuko bize sana kuzalisha, mwingine anakula raha tu. Huyu mchapa kazi akisafiri huku nyuma huyu mvivu anaenda kwenye akaunti na kutoa pesa na kufanya matanuzi. Baadaye biashara kama hii huishia chini.
3. KUAJIRI WATU WASIO SAHIHI
Kuajiri watu wasiofaa katika biashara yako husababisha matatizo makubwa kwa mjasiriamali yeyote. Walewale ambao unadhani ndiyo wangekusaidia kwenda mbele ndiyo haohao wanaoweza kuwa mstari wa mbele kukudidimiza. Chukua muda wa kutosha kutafuta watu sahihi.
Fanya usaili zaidi ya mara mbili kwa kila unayetaka kumwajiri kama mfanyakazi wako. Furaha au huzuni kubwa kwa mjasiriamali hutokana na wafanyakazi ulionao. Hakikisha wewe mwenyewe kwanza ni mtu mzuri na unastahili kuwaongoza wengine kwa haki, hekima, usawa nk.
4. KUKOSA MTAJI WA UHAKIKA
Wakati naanza ujasiriamali miaka saba iliyopita, katika baadhi ya vitu vilivyokuwa vikinisumbua sana mojawapo lilikuwa ni hili. Mara kwa mara ofisi yangu ilikuwa inakaukiwa pesa za uendeshaji wa shughuli zake mbalimbali. Nilikuja kupata upenyo baada ya kuja kutambua kuwa pesa ya biashara na pesa yangu binafsi vilikuwa ni vitu viwili tofauti na sikutakiwa kuvichanganya.
Hivyo hata kama moja tu ya mambo yaliyotajwa hapo juu hayadhibitiwi vyema, lina uwezo wa kufanya biashara yako ianguke ndani ya miezi au miaka kadhaa ijayo. Ndiyo maana benki hazitaki kuzikopesha biashara mpya, zinatambua kuwa uwezekano wa kushindwa ni mkubwa sana kuliko kushinda kwa mjasiriamali mchanga au anayeanza. Ndiyo maana wanataka kushughulika na biashara endelevu zilizosimama na zenye vigezo vyote sahihi.
Msomaji, nimechukua muda mrefu kukuonesha sababu mbalimbali zinazofanya biashara nyingi mpya kuanguka na jinsi ambavyo benki zinafahamu kwa kina ukweli huu na ndiyo maana huwa haziko tayari kumsaidia mjasiriamali anayeanza biashara kwa mara ya kwanza. Lakini pamoja na haya yote itakupasa kufikiri zaidi kama kiongozi shujaa wa biashara yako.
Wajasiriamali waliofanikiwa sana huwa wanafikiri kiuwezekano zaidi, kwa lugha ya kitaalamu wanaitwa possibility thinkers.
kwa kuwa wanafikiria zaidi kuhusu yale yanayowezekana kuliko yasiyowezekana kuhusiana na maisha yao yajayo.
Viongozi hawa huwa wanaamini kwamba yote yanawezekana kabla hata hawajaanza, halafu ndipo huanza biashara zao kwa imani. Jukumu lako kubwa itakuwa ni kuwa possibility thinker pia, kisha baada ya hapo itakupasa kubadilisha kuamini kwako kuwe maono halafu maono hayo yawekwe kwenye malengo na mipango inayotekelezeka na kupimika kirahisi.
Jambo la msingi ni kutambua kuwa japo asilimia zaidi ya 90 ya biashara mpya hushindwa, habari njema ni kwamba zaidi ya 90% ya wajasiriamali wanaojaribu kwa mara ya pili kwenye biashara nyingine baada ya kushindwa kwa mara ya kwanza, huwa wanafanikiwa katika biashara zao za mara ya pili.
Lakini mchungaji mmoja wa makanisa makubwa kuliko yote Marekani na moja kati ya wahubiri maarufu kuliko wote duniani, Joel Osteen husema kwamba, 80% ya wajasiriamali wote walioshindwa kwa mara ya kwanza walipoanzisha biashara zao, huwa kamwe hawajaribu tena kwa mara nyingine kufungua biashara kwa mara ya pili. Wengi kama tunavyojua huishia kurudi tena kwenye ajira, au kwenye umama wa nyumbani au hukimbilia vyuoni kujiendeleza kielimu n.k.
Tumalizie kipengele hiki cha kupata mtaji kupitia taasisi za kibenki kwa kusema kwamba ni njia mojawapo ya kuweza kukusaidia kupata mtaji wa biashara yako kama utakuwa umezingatia vigezo vifuatavyo ambavyo mameneja wa benki wataviangalia kwa makini na watahitaji uwe umevitimiza barabara.
Watu wengi wamenufaika kwa kupitia mikopo ya kibenki ambayo imewafanya wawe mabilionea hapa kwetu Tanzania na wamewekeza katika biashara za kila aina kama vituo vya mafuta, mabasi ya usafirishaji abiria, hoteli kubwa, shule za msingi na sekondari n.k. Kama wao wameweza na wewe utaweza, kubali kuanza kidogo. Haya, vigezo hivyo ni kama ifuatavyo;
1. Mtaji ulionao: Watu wa benki huvutiwa sana kuona kwamba tayari una mtaji kwenye biashara yako. Na kama ni biashara mpya unaweza kuwa na ushawishi mkubwa ikiwa utaonesha kwamba na wewe kama mjasiriamali uko tayari kuwekeza pesa yako binafsi.
2. Mtiririko wa fedha: Hakuna kitu kinachowavutia wenye mabenki kama biashara ambayo ina mtiririko mzuri wa kifedha (healthy positive cash flow) Kwa lugha nyepesi, ukiwa unatunza mahesabu yako na kila kitu kiko peupe kuhusiana na pesa inavyoingia na kutoka huku ukitengeneza faida, utakuwa umewavutia wakopeshaji.
3. Maadili: Kwa lugha nyingine, je umekuwa na uhusiano mzuri na asasi husika au zingine za kifedha? Vipi una rekodi ambazo si safi za ulipaji kama vile bili za umeme, maji, TRA n.k? Hivi vyote huwapa wakopeshaji picha halisi ya maadili ulinayo.
4. Dhamana: Mara nyingi dhamana huja mwishoni baada ya kuyaangalia mambo hayo ya juu. Kiasi cha mkopo unachohitaji kitasababisha kuamua ni aina gani ya dhamana itahitajika. Mara nyingi benki hupendelea dhamana zisizohamishika kama nyumba, viwanja n.k.
5. Masharti/Makubaliano: Ukiwa umefanikiwa katika yote ya hapo juu, mwisho wao huangalia kama utakubaliana na masharti mbalimbali ya mkopo wao ikiwemo kiwango cha riba, namna ya ulipaji, muda wa kumaliza kulipa mkopo huo n.k.

إرسال تعليق