WANAJESHI
wapatao wanane wanadaiwa kuwatesa na kuwapiga vijana watatu katika eneo
la Ubungo Kibangu, Dar es Salaam pasipokuwa na sababu maalumu.
Wakizungumza
na mwandishi wetu jana, vijana hao walieleza kuwa walikamatwa na
wanajeshi hao na kupelekwa porini kisha wakateswa na kupigwa kwa zaidi
ya saa tano bila kufahamu kosa lao na hata walipohoji waliambiwa
hawaruhusiwi kuhoji wanajeshi.
Mmoja
wa vijana hao, Sebastian Mlekano (40) alisema saa 12:30 jioni ya
Januari 13 mwaka huu katika eneo la Ubungo Kibangu karibu na kambi ya
jeshi ya Makoka, alisimamishwa na wanajeshi wapatao wanane na kuamuriwa
wakae chini.
“Nilikuwa
napita njia iliyopo karibu na jeshi nikakutana na kundi la wanajeshi
wapatao wanane na wakaniambia kaa chini. Nikawauliza nimefanyaje?
Wakanijibu wewe huoni sisi ni wanajeshi hupaswi kuuliza umefanya nini.”
“Baada
ya hapo wakaniambia wewe tufuate, hatua chache mbele tukakutana na
kijana mmoja na alipoona mimi nipo chini ya ulinzi aliamua kukimbia na
wakamkimbiza na kumkamata kisha wakatupeleka porini. Tulipofika kule
muda mfupi wakamleta na mtu mwingine tukafikia idadi ya watu watatu."
Aliendelea kuongeza kuwa,
“Tulipofikishwa porini tukaanza kufanyishwa mazoezi magumu na kupigwa
sana kama ambavyo unaona majeraha haya yote. Nilizimia kwa muda na
nilipopata fahamu kipigo kiliendelea kama kawaida kwa muda usiopungua
saa tano,” alisema Mlekano.
Alisema walipoona wamewaumiza sana waliamua kuwaachia huru na wakarudi majumbani kwao.
Walipofika
barabarani kutokea porini kwenye mateso, walikutana na kundi kubwa la
watu waliokuwa wanawafuata kwani mama mzazi wa Godfrey Mchari alikuwa
amemtuma mwanawe dukani na alipoona amechelewa aliamua kuongozana na
majirani kujua hatma ya mtoto wake.
“Godfrey
alipomwona mama yake na kundi hilo la watu waliotufuata alianguka chini
akazimia, wakambeba na kumpeleka hospitali moja kwa moja. Mimi na
mwenzangu kila mtu alikwenda kwake,” alisema Mlekano. Baada ya hapo
Mlekano alisema alienda kutoa taarifa kituo cha Polisi cha Mwongozo na
kupatiwa fomu ya matibabu.
Pia
analalamika kupoteza kadi ya bima ya afya, leseni ya gari pamoja na
kiasi cha fedha. Godfrey Mchari kwa upande alisema alitumwa dukani na
mama yake kwenda kutuma pesa dukani kwa wakala wa M-pesa na kabla
hajafika alikutana na wanajeshi waliomwamrisha akae chini na ndipo yeye
akaamua kukimbia.
Akijibu
tuhuma hizo pamoja na hatua zilizochukuliwa na Jeshi kufuatia kadhia
hiyo, msemaji wa jeshi Meja Joseph Masanja alisema taarifa hiyo bado
haijawafikia na kuahidi atafuatilia jambo hilo ikiwa ni pamoja na
kuonana na walalamikaji ili kulipatia ufumbuzi na ufafanuzi zaidi.
“Hizo taarifa bado hazijatufikia na nashukuru kwa kunipa taarifa hii, tutafuatilia na kutoa taarifa kamili wiki ijayo” alisema Masanja
Post a Comment