Dar es Salaam. Wakati safari ya kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba mwaka huu ikipamba moto, kumeibuka makundi ya watu yaliyofungia
akaunti katika mitandao ya kijamii yakiwaunga mkono baadhi ya wanasiasa
waliotangaza au wanaotajwa kuwa na nia ya kugombea urais ya
kuwashambulia washindani wao.
Kila kundi limejipatia wafuasi wengi ambao
wanaonyesha kumkubali mwanasiasa husika wanayedhani anafaa kuwa rais wa
Tanzania endapo atapitishwa na chama chake na kupigiwa kura na wananchi.
Hata hivyo, wasomi na wachambuzi wanaonya kuwa
pamoja na njia hii kuwa ya haraka kuwafikia wapigakura walio wengi ambao
ni vijana na wanawake, inatakiwa kutumika kwa uangalifu la sivyo
inaweza kusababisha machafuko.
Makundi yenyewe
Makundi hayo, mengi yakipatikana katika mitandao
ya Facebook, Twitter na WhatsApp yanafanya kazi ya kuwanadi wanasiasa na
kubainisha shughuli mbalimbali wanazozifanya kila siku wawapo katika
ziara zao za binafsi, za kiserikali au kichama katika maeneo mbalimbali
nchini.
Baadhi ya kurasa za makundi hayo zenye wafuasi
wengi ni pamoja na ule wa ‘Team Lowassa’, kundi linalomuunga mkono
Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ambao hadi jana ulikuwa na wafuasi
46,124 ambao wanaweza kupata habari mbalimbali zinazomhusu kiongozi
huyo.
Hata hivyo, mbunge huyo ambaye pia aliwahi kuwa
waziri mkuu, hivi karibuni alikaririwa na gazeti hili akiikana moja ya
akaunti za Twitter iliyokuwa imechapisha taarifa zilizomkariri
akizungumzia suala la ufisadi wa escrow.
Akizungumzia kurasa hizo, Msaidizi wa Lowassa,
Abubakar Liongo alisema akaunti hizo zinatengenezwa na marafiki na
kusisitiza kwamba kiongozi huyo hahusiki nazo kwa namna yoyote.
“Hawa ni marafiki tu, huwezi kuwazuia kufanya
wanachotaka kufanya, sisi tumeshatoa taarifa kuwa hizi hatuhusiki nazo,”
alisema Liongo.
Kundi jingine linajitambulisha kama ‘Team Hamis
Kigwangalla’ linalomuunga mkono Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla na
mpaka kufikia jana lilikuwa na wafuasi 9,893. Hili ni kundi la pili
kuwa na wafuasi wengi katika mtandao wa Facebook baada ya lile la Team
Lowassa.
Ukurasa mwingine umeanzishwa na watu wanaomuunga
mkono Mbunge wa Bumbuli na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba. Ukurasa huu umepewa jina ‘January Makamba –
The next President’ na hadi jana ulikuwa na wafuasi 7,075.
Wanasiasa wengine wanaohusishwa na mitandao hiyo
ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
ambaye mbali na akaunti yake kwenye WhatsApp, ukurasa wa marafiki zake
kwenye Facebook wenye jina la ‘Bernard Membe Fans Page’ umefikisha
wafuasi 5,120.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق