Arusha. Simba wanane waliotoka nje ya Hifadhi ya Taifa ya
Tarangire na kuingia eneo la Kijiji cha Kibaoni wilayani Babati mkoani
Manyara, wameuawa kwa kuchomwa mikuki na wananchi.
Kijiji cha Kibaoni kipo hatua chache kutoka
Hifadhi ya Tarangire ambayo ni mojawapo ya vivutio vya kitalii na mara
nyingi wanyamapori huzagaa kijijini hapo, hasa nyakati za masika kuepuka
majani marefu hifadhini.
Tukio hilo linaloelezewa kuwa ni janga kubwa kwa
sekta ya uhifadhi na utalii nchini, lilitokea jana alfajiri na hadi Saa
6.00 mchana na mizoga saba ya Simba ilipatikana, huku mmoja akiaminika
kufia kwenye vichaka baada ya kukimbia alipojeruhiwa.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu
ameziagiza mamlaka zinazohusika kuwasaka na kuwatia mbaroni wote
waliowahamasisha na kuwaongoza wakazi wa kijiji hicho kuwaua Simba hao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha
jana, Nyalandu alitoa maagizo kwa polisi kuchunguza uhalali wa bunduki
inayomilikiwa na mmoja wa wakazi wa kijiji hicho iliyotumika kuwaua
Simba wawili kati ya saba.
“Kuua idadi kubwa ya Simba kwa wakati mmoja, tena
katika siku ya kwanza ya Mwaka Mpya ni jambo la kusikitisha na
linastahili kulaaniwa na wote wenye mapenzi mema na uhifadhi ndani na
nje ya nchi,” alisema Nyalandu na kuongeza:
“Hatuwakamati wakazi wote 100 walioshiriki kuwaua
simba hawa, bali tutashughulika na wale waliochochea mauaji ili kutoa
fundisho kwa wale wanaochukua sheria mkononi kwa kuwaua wanyamapori,”
alisema Nyalandu.
Hifadhi ya Taifa ya Tarangire inakadiriwa kuwa na
Simba kati ya 200 hadi 250 na Tembo wanaokadiriwa kufikia 3,000 na
wanyama wengineo zaidi ya 10,000.
Mmoja wa wanakijiji aliyezungumza kwa sharti la
kutotajwa jina gazetini kwa sababu za kiusalama, alisema Simba hao
waliuawa baada ya kudaiwa kumla punda kihongwe kwenye moja wa maboma ya
wakazi wa kijiji hicho ambao ni jamii ya wafugaji wa Kimasai.
“Usiku kundi la Simba zaidi ya 12 walionekana
wakizunguka katika maeneo ya karibu na kambi ya Watalii ya Zion
Campsite. Ilipofika alfajiri, watu wakaanza kupiga mayowe kuashiria
hatari baada ya Simba hao kusambaa kijijini,” alisema na kuongeza;
“Kelele hizo ziliwashtua Simba na kuwafanya waanze
kuunguruma, hali iliyozua taharuki na vijana (Morani), wakaanza
kupambana nao na kuwaua mmoja baada ya mwingine hadi kufikia Simba saba
na mmoja alikimbia akiwa na mkuki mwilini.”
إرسال تعليق