Katuni.
Katika taarifa hiyo ambayo ni mojawapo ya habari zilizokuwamo kwenye gazeti hili toleo la jana, ilielezwa kuwa hatua hiyo ya wakulima inatokana na sababu kadhaa, mojawapo ikiwa ni janga lililowakumba la kupoteza zaidi ya hekta 4,079.6 zenye jumla ya tani 171,000 za miwa baada ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba yao. Thamani halisi ya miwa hiyo imetajwa kuwa ni takriban Sh. bilioni 7.7.
Mmoja wa viongozi wa Chama cha Wakulima wa Nje wa Miwa (Moa), alisema uharibifu huo ulitokea katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2011 hadi 2013. Na kwamba hali hiyo iliwafanya wakulima wengi wa miwa waogope kuwekeza zaidi nguvu zao, muda na rasilimali fedha msimu huu wakihofia kupata hasara kama ilivyotokea miaka hiyo mitatu iliyopita.
Aliongeza kwamba hivi sasa hali ni mbaya. Mifugo imekuwa ikiingia kwa makundi kwenye mashamba yao na kuwasababishia uharibifu mkubwa.
Alijitolea mfano yeye mwenyewe, akisema amepoteza tani 2,700 za miwa yake iliyokuwa shambani licha ya kwamba aliweka walinzi kwani kundi kubwa la wafugaji liliwazidi nguvu (walinzi hao), kutishia kuwapiga na mwishowe kuingiza mifugo hiyo iliyomsababishia hasara kubwa.
Hakika, taarifa hizi siyo nzuri. Ni za kuwakatisha tamaa wakulima hao wa miwa na kwa namna yoyote ile, jitihada za ziada zinatakiwa kuchukuliwa haraka katika kufanya uchunguzi wa kina na kushughulikia tatizo hili.
Kwa namna ilivyo, sisi tunaamini kwamba suala hili limo ndani ya uwezo wa uongozi wa wilaya. Ni wazi kwamba hadi kufikia sasa, zipo taratibu kadhaa za kushughulikia suala hilo katika ngazi ya kijiji na hata kata. Na kama kote huko imeshindikana, wahusika wanapaswa kufuata utaratibu kwa kulifikisha kwa uongozi wa juu wilayani na mwishowe mkoa. Ni matumaini yetu kuona kuwa watu waliopewa mamlaka ya kuongoza maeneo hayo wanatekeleza wajibu wao sasa na siyo kusubiri hali iwe mbaya ndipo wafuatilie suala hili.
Sisi tunasisitiza hili kutokana na kile kilichoonekana katika mfululizo wa matukio kadhaa ya aina hiyo nchini ambayo chanzo chake huwa ni chokochoko kama hizi za kuwapo kwa tuhuma za kuingiza mifugo kwenye mashamba na kusababisha hasara. Kuna mauaji ya watu wasio na hatia yameshatokea mara kadhaa kwenye maeneo ya Kilosa mkoani Morogoro, Kiteto mkoani Arusha, Rufiji mkoani Pwani na pia Mvomero kwenyewe. Mashamba, nyumba na mifugo yenye thamani ya mamilioni ya fedha ni miongoni mwa hasara zilizoripotiwa kutokea katika maeneo yaliyowahi kukumbwa na mapigano ya wakulima na wafugaji.
Ni kawaida pia kuona kuwa maeneo yanayokumbwa na migogoro ya wakulima na wafugaji kukumbwa na athari za kiuchumi. Ni kwa sababu amani hutoweka. Watu hukosa utulivu wa kuwawezesha kuendelea na shughuli zao za uzalishaji kama kulima, kufuga na kufanya biashara. Matokeo yake, njaa huwa huwakumba.
Cha kusikitisha ni kwamba athari hizi za migogoro ya wakulima na wafugaji zingali zikinyemelea kwenye maeneo haya ya mashamba ya miwa. Kama wakulima wa miwa wataendelea kuogopa kujihusisha na kilimo hicho, maana yake ni kwamba uchumi wao utayumba. Kiasi cha miwa inayohitajika kwa uzalishaji wa sukari kwenye Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa kitapungua. Hapo, athari hizi zitakwenda mbali zaidi. Ajira iliyopo kwenye uzalishaji wa bidhaa hii itatetereka na mapato ya nchi kupitia kodi na aina nyingine za ushuru yatapungua.
Kwa kutambua yote hayo, ni wazi kwamba sasa kuna kila sababu kwa viongozi wa Wilaya ya Mvomero kushughulikia madai hayo ili kuzuia maafa yanayoweza kutokea pindi mgogoro huu wa wakulima wa miwa na wafugaji ukasababisha mapigano na pia kuzuia athari hasi za kiuchumi zinazoweza kutokea sasa baada ya wakulima wa miwa kuanza kujiondoa kwenye kilimo hicho.
Viongozi wa Mvomero wahakikishe kwamba wanakutanisha viongozi wa pande zote, kwa maana ya wakulima na wafugaji na kupata suluhu kabla hali haijawa mbaya. Ikumbukwe kuwa kushughulikia migogoro ya aina hii katika hatua za awali ni bora kuliko kusubiri athari zake kwa usalama na uchumi.
CHANZO:
NIPASHE
إرسال تعليق