Wapiga ramli wapinga agizo la serikali la kuwataka kutokujihusisha na shughuli hiyo.

Siku chache baada ya serikali kupiga marufuku upigaji ramli nchini kwa madai kuwa inachangia kwa asilimia kubwa mauaji na ukatwaji wa viungo vya watu wenye albinism, baadhi ya waganga wanaojishughulisha na vitendo hivyo wamepinga agizo hilo huku jukwaa la tiba asili likipongeza hatua hiyo ya serikali.
Kufuatia agizo hilo la serikali ITV ilitaka kufahamu wahusika na wadau mbalimbali wa tiba za asili wamelipokeaje agizo hilo ambapo imefanikiwa kuzungumza na mzee Shabani Rajabu ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha waganga na wakunga wa jadi nchini na anajishughulisha na upigaji ramli ambapo amesema serikali inatakiwa kuwa makini katika kuendesha zoezi hilo kwani yenyewe inahusika kutoa vibali na kuongeza kuwa siyo ramli zote ni chonganishi.
Kwa upande wa jukwaa la tiba asili tanzania mbali na kupongeza agizo hilo la serikali wameitaka kwanza kutoa elimu kwa njia mbalimbali kwa wananchi kwani asilimia kubwa wanahusisha ramli kama sehemu ya matibabu au kugundua magonjwa lakini pia baadhi ya watawala wamekuwa wakitumia ramli hizo wakidhani zitaweza kuweka mambo yao sawa katika nyadhifa zao huku wakiitaka serikali kuwa makini katika kutoa vibali kwa waganga hao
Agizo la kupiga marufuku upigaji ramli nchini lilitolewa jijini dar es salaam hivi karibuni na waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mh. Mathias Chikawe ambaye alisema timu ya watu sita wakiwemo askari na watu wenye albinisim itaendesha operesheni maalum ya kusaka watu hao kama njia mojawapo ya kukabiliana na tatizo la mauaji ya albino hapa nchini  ambayo alikiri kuongezeka mwishoni mwa mwaka jana.

Post a Comment

Previous Post Next Post