Siku chache baada ya serikali kupiga marufuku upigaji ramli nchini
kwa madai kuwa inachangia kwa asilimia kubwa mauaji na ukatwaji wa
viungo vya watu wenye albinism, baadhi ya waganga wanaojishughulisha na
vitendo hivyo wamepinga agizo hilo huku jukwaa la tiba asili likipongeza
hatua hiyo ya serikali.
Kufuatia agizo hilo la serikali ITV ilitaka kufahamu wahusika na
wadau mbalimbali wa tiba za asili wamelipokeaje agizo hilo ambapo
imefanikiwa kuzungumza na mzee Shabani Rajabu ambaye pia ni mwenyekiti
wa chama cha waganga na wakunga wa jadi nchini na anajishughulisha na
upigaji ramli ambapo amesema serikali inatakiwa kuwa makini katika
kuendesha zoezi hilo kwani yenyewe inahusika kutoa vibali na kuongeza
kuwa siyo ramli zote ni chonganishi.
Kwa upande wa jukwaa la tiba asili tanzania mbali na kupongeza
agizo hilo la serikali wameitaka kwanza kutoa elimu kwa njia mbalimbali
kwa wananchi kwani asilimia kubwa wanahusisha ramli kama sehemu ya
matibabu au kugundua magonjwa lakini pia baadhi ya watawala wamekuwa
wakitumia ramli hizo wakidhani zitaweza kuweka mambo yao sawa katika
nyadhifa zao huku wakiitaka serikali kuwa makini katika kutoa vibali kwa
waganga hao
Agizo la kupiga marufuku upigaji ramli nchini lilitolewa jijini dar
es salaam hivi karibuni na waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mh. Mathias
Chikawe ambaye alisema timu ya watu sita wakiwemo askari na watu wenye
albinisim itaendesha operesheni maalum ya kusaka watu hao kama njia
mojawapo ya kukabiliana na tatizo la mauaji ya albino hapa nchini
ambayo alikiri kuongezeka mwishoni mwa mwaka jana.
إرسال تعليق