Mapigano ya wakulima na Wafugaji: Mmoja Auawa, 14 Wajeruhiwa Vibaya


Mgogoro kati ya Wakulima na Wafugaji katika bonde la Mgongola , wilayani Mvomero mkoani Morogoro umeibuka tena na kusababisha kifo cha mkulima mmoja na wengine 14 kujeruhiwa.
 
Waliojeruhiwa wamekatwa sehemu mbalimbli za miili yao na mapanga na sime za wafugaji.
 
Kati ya wakulima waliojeruhiwa kwenye tukio hilo lilitokea jioni ya Januari 16, mwaka huu ni pamoja na aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Ally Ambilikila na familia yake .
 
Hata hivyo baada ya kumvamia walimpora fedha taslim Sh milioni tatu na kumchomea moto nyumba iliyokuwa ndani ya eneo la shamba lake.
 
Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Leonald Paulo, alithibitisha kutokea kwa mapigano hayo na kumtaja aliyeuawa kuwa Abdallah Shomari (27) mkazi wa Msamvu Manispaa ya Morogoro ambaye alikuwa ndani ya shamba hilo na kupigwa kwa marungu na wafugaji hao.
 
Kamanda Leonald amesema katika tukio hilo tayari jeshi la Polisi limefanikiwa kuwakamata wafugaji wawili wa Kimasai ambao ni Kisaingwa Mbingwa na Rashid Saliku wote wakazi wa kijiji cha Kambala wilayani Mvomero.
 
Alisema kwamba siku ya tukio wakulima waliamua kwenda kuandaa mashamba na baadaye wafugaji walienda katika eneo hilo na kutokea mzozo mkubwa kipindi cha mchana ambapo jioni yake kukatokea mapigano hayo.
 
Kwa upande wa Kamanda mstaafu Ambalikila akielezea tukio hilo la kuvamiwa na wafugaji , alisema kuwa siku hiyo walienda katika bonde hilo ambalo wanalima tangu miaka 60 iliyopita kwa ajili ya kuanza kutayarisha mashamba ya mpunga kwa msimu huu.
 
Alisema kuwa wakati wakiendelea kulima kwa kutumia trekta la kukodi ghafla lilitokea kundi kubwa la jamii ya wafugaji wa Kimasai wa kijiji cha Kambala na kuvamia eneo hilo.
 
Alisema mara baada ya kuwavamia wafugaji hao waliwapiga kwa kutumia sime, fimbo na mapanga sehemu mbalimbali akiwemo yeye pamoja na familia ya watu kumi waliokuwa shambani kwa ajili ya matayarisho ya shamba.
 
Kamanda huyo mstaafu wakati wafugaji hao wakiendelea kuwapiga baadhi yao walimpora fedha taslimu Sh milioni 3, simu na kuchoma magunia 20 ya mbegu ya mpunga iliyokuwa tayari kwa kupandwa katika shamba lake.
 
Hata hivyo alisema baada ya tukio hilo wafugaji hao waliondoka na wao kupata msaada kutoka kwa wananchi na kuwafikisha kituo cha Polisi na baadaye kufikishwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu.
 
Naye Said Ambilikila ambaye ni mtoto wa Kamanda huyo mstaafu aliyelazwa katika Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro, alisema kuwa alipigwa kichwani na mkononi na wafugaji hao kwa kutumia silaha hizo za jadi baada ya kuvamiwa wakiwa katika shamba lao.
 
Kwa upande wa Costa Augustino mkazi wa kijiji cha Dihombo wilayani Mvomero ambaye naye amelazwa akipatiwa matibabu kutokana na kukatwa mapanga katika mikono yake yote miwili na sehemu ya kichwani alisema baada ya kupambana na wafugaji hao alilazimika kutumia mbinu za kujifanya kuwa amekufa na wafugaji hao kuondoka.
 
Alisema kuwa baada ya wafugaji hao kuona kuwa amekufa walitawanyika na yeye alijivuta mpaka katika kibanda na baadaye kuja kuokolewa na askari wa jeshi la Polisi waliofika eneo hilo baada ya kupata taarifa.
 
Baadhi ya majeruhi wengine waliolazwa katika hospitali hiyo ni Rajabu Ally, Mohamed Ramadhan na Ramadhani Salum wote wakazi wa kata ya Kinguruwila manispaa ya Morogoro.
 
Wakizungumza wadini hapo Mohamed Ramadhan alisema baada ya kupigwa aliporwa na wafugaji kiasi cha Sh 150,000 pamoja na simu ya mkononi, wakati Ramadhani Salum alidai kuporwa kiasi cha Sh 850,000 na kuchomewa pikipiki pamoja na nyumba yake iliyokuwa shambani kwake.
 
Msimamizi Mkuu wa Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro,Elias Kilela, alithibitisha kupokea majeruhi saba waliohamishiwa katika hospitali hiyo baada ya kujeruhiwa na Wafugaji katika Bonde la Mgongola.
 
Alisema kuwa majeruhi hao wamelazwa wadi namba moja hospitalini hapo huku wakiwa wamekatwakatwa na mapanga katika maeneo yao mbalimbali ya mwili na wanaendelea vizuri baada ya kuanza kupatiwa matibabu huku mmoja ambaye ni Kamanda mstaafu wa Polisi akiruhusiwa.
 
Awali Mwenyekiti wa kijiji cha Mkindo Patrick Longomeza ambaye ni miongoni mwa wakulima wanaolima katika bonde hilo la Mgongola alithibitisha baadhi ya wakulima kutoka katika kijiji chake kujeruhiwa na wafugaji baada kuvamiwa wakiwa katika bonde hilo.
 
Alisema wakulima hao walienda katika bonde hilo kwa ajili ya kuandaa mashamba ya mpunga ambalo wamekuwa wakilima kwa muda mrefu.
 
Alisema kuwa baada ya kupata taarifa walienda katika eneo la tukio na kuwakimbiza katika hospitali za Bwagara na wengine kituo cha afya cha Mvomero huku baadhi wakiwakimbiza katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro ambako baadhi yao wamelazwa kwa ajili ya matibabu.

Post a Comment

أحدث أقدم