Geita. Mtoto mwingine mwenye ulemavu wa ngozi
(albino) ametekwa mkoani Geita, likiwa ni tukio la pili ndani ya kipindi
kisichozidi siku 50.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Joseph Konyo
alimtaja mtoto aliyetekwa kuwa ni Yohana Bahati mwenye umri wa mwaka
mmoja na miezi sita, kwamba alitekwa usiku wa kuamkia juzi akiwa
nyumbani kwao na wazazi wake.
Hili ni tukio ni la pili kutokea katika mikoa ya
Kanda ya Ziwa, baada ya tukio la awali kutokea kijiji cha Ndami wilayani
Kwimba mkoani Mwanza, ambako mtoto Pendo Emmanuel mwenye umri wa miaka
minne alitekwa na watu wasiojulikana usiku wa Desemba 27, mwaka jana na
hadi sasa bado hajapatikana wala watekaji wa mtoto huyo hawajakamatwa.
Hali hiyo inatokea huku kukiwa na agizo la Mkuu wa
Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo la Januari 6, alipotoa siku tano kwa
wanakijiji wa Ndami na kikundi cha ulinzi cha jadi cha sungusungu
wilayani Kwimba kwamba ndani ya kipindi hicho mtoto Pendo awe
amepatikana.
Wakati utekelezaji wa agizo hilo ukiwa haujatimia
tukio lingine la utekaji limetokea mkoani Geita usiku wa kuamkia juzi
wakati mama wa mtoto huyo (Yohana), Ester Jonasi (30) akiwa katika
harakati za kuandaa chakula cha usiku.
Tukio hilo lilitokea kwenye kitongoji cha
Ilyamchele, Kijiji cha Ilelema wilayani Chato mkoani Geita, ambapo watu
wanaodaiwa kufanya unyama huo walikuwa wawili na walivamia nyumbani kwa
wazazi wa mtoto huyo wakiwa na mapanga na kisha kutoweka naye
kusikojulikana baada ya kuwazidi nguvu wazazi wake.
Kamanda Konyo alisema watu hao wakiwa na mapanga
baada ya kufika katika familia hiyo, walimteka mama yake na katika
kunyang’anyana mtoto walilazimika kutumia mapanga kwa kumjeruhi mama wa
mtoto huyo.
Familia hiyo ina watoto watatu wote albino ambapo
wakati mtoto mwingine anatekwa kaka yake alikuwa kwa jirani anacheza na
aliporejea nyumbani alikuta tukio limetokea.
“Katika purukushani hizo waharifu hao walimjeruhi
mama wa mtoto huyo...mikononi, kichwani na begani na amelazwa kwenye
hospitali ya Wilaya ya Geita kwa matibabu.
“Kilichotokea ni kwamba watu wa familia ya mtoto
huyo...Inaishi porini ambako ni eneo la hifadhi ambako hapatakiwi kuishi
watu..kutokana na mazingira hayo ilikuwa siyo rahisi kuwamakata watu
hao.”
Konyo alisema pamoja na juhudi za wananchi na
polisi kufika eneo la tukio hazikuzaa matunda kuwakamata watu hao,
juhudi za kuwatafuta watuhumiwa hao zinaendelea na hivyo kutoa wito kwa
wananchi kushirikiana kuwasaka.
“Tukio hilo ni la kwanza katika mkoa wetu wa
Geita...Limetuweka katika mazingira magumu sana lakini tumejipanga timu
ya makachero inaendelea kuchunguza na kwamba tutahakikisha huyo mtoto
anarudi.”
- Mwananchi Hapa
- Mwananchi Hapa
Post a Comment