Albino mwingine atekwa Kanda ya Ziwa

Geita. Mtoto mwingine mwenye ulemavu wa ngozi (albino) ametekwa mkoani Geita, likiwa ni tukio la pili ndani ya kipindi kisichozidi siku 50.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Joseph Konyo alimtaja mtoto aliyetekwa kuwa ni Yohana Bahati mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi sita, kwamba alitekwa usiku wa kuamkia juzi akiwa nyumbani kwao na wazazi wake.
Hili ni tukio ni la pili kutokea katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, baada ya tukio la awali kutokea kijiji cha Ndami wilayani Kwimba mkoani Mwanza, ambako mtoto Pendo Emmanuel mwenye umri wa miaka minne alitekwa na watu wasiojulikana usiku wa Desemba 27, mwaka jana na hadi sasa bado hajapatikana wala watekaji wa mtoto huyo hawajakamatwa.
Hali hiyo inatokea huku kukiwa na agizo la Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo la Januari 6, alipotoa siku tano kwa wanakijiji wa Ndami na kikundi cha ulinzi cha jadi cha sungusungu wilayani Kwimba kwamba ndani ya kipindi hicho mtoto Pendo awe amepatikana.
Wakati utekelezaji wa agizo hilo ukiwa haujatimia tukio lingine la utekaji limetokea mkoani Geita usiku wa kuamkia juzi wakati mama wa mtoto huyo (Yohana), Ester Jonasi (30) akiwa katika harakati za kuandaa chakula cha usiku.
Tukio hilo lilitokea kwenye kitongoji cha Ilyamchele, Kijiji cha Ilelema wilayani Chato mkoani Geita, ambapo watu wanaodaiwa kufanya unyama huo walikuwa wawili na walivamia nyumbani kwa wazazi wa mtoto huyo wakiwa na mapanga na kisha kutoweka naye kusikojulikana baada ya kuwazidi nguvu wazazi wake.
Kamanda Konyo alisema watu hao wakiwa na mapanga baada ya kufika katika familia hiyo, walimteka mama yake na katika kunyang’anyana mtoto  walilazimika kutumia mapanga kwa kumjeruhi mama wa mtoto huyo.
Familia hiyo ina watoto watatu wote albino ambapo wakati mtoto mwingine anatekwa kaka yake alikuwa kwa jirani anacheza na aliporejea nyumbani alikuta tukio limetokea.
“Katika purukushani  hizo waharifu hao walimjeruhi mama wa mtoto huyo...mikononi, kichwani na begani na amelazwa kwenye hospitali ya Wilaya ya Geita kwa matibabu.
“Kilichotokea ni kwamba watu wa familia ya mtoto huyo...Inaishi porini ambako ni eneo la hifadhi ambako hapatakiwi kuishi watu..kutokana na mazingira hayo ilikuwa siyo rahisi  kuwamakata  watu hao.”
Konyo alisema pamoja na juhudi za wananchi na polisi kufika eneo la tukio hazikuzaa matunda kuwakamata watu hao, juhudi za kuwatafuta watuhumiwa hao zinaendelea na hivyo kutoa wito kwa wananchi kushirikiana kuwasaka.
“Tukio hilo ni la kwanza katika mkoa wetu wa Geita...Limetuweka katika mazingira magumu sana lakini tumejipanga timu ya makachero inaendelea kuchunguza na kwamba tutahakikisha  huyo mtoto anarudi.”
- Mwananchi Hapa

Post a Comment

أحدث أقدم