Dar es Salaam. Sakata la Rais wa Serikali ya
Wanafunzi ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dar es Salaam, Ramadhan
Kilungi kudaiwa kughushi saini na kuiba Sh32 milioni katika akaunti ya
Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho (Cobeso), limechukua sura mpya baada
ya baadhi ya wanafunzi kudai kuwa utawala wa chuo hicho unahusika.
Habari kutoka ndani ya chuo hicho zilizolifikia
gazeti hili zinaeleza kuwa kabla ya Kilungi kuchota fedha hizo Februari
7, mwaka huu, mwanzoni mwa Januari alichota tena Sh12 milioni katika
akaunti hiyo kwa ajili ya safari ya Bunge la wanafunzi lililotembelea
vikao vya Bunge mjini Dodoma.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kwa nyakati tofauti,
kuanzia Oktoba 2, mwaka jana hadi Januari 26 mwaka huu, Bunge la
wanafunzi limekuwa likiuandikia barua utawala wa chuo hicho kutaka
ufafanuzi wa matumizi ya fedha na kushinikiza vifanyike vikao, lakini
utawala ulizuia.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki alisema kwa sasa Kilungi yuko nje kwa dhamana
na uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili unaendelea.
“Kwa sasa yupo nje kwa dhamana na uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani,” alisema Nzuki.
Kilungi alipotafutwa na gazeti hili jana, mazungumzo yalikuwa hivi;
Mwananchi: Pole kwa matatizo yaliyokupata.
Kilungi: Asante.
Mwananchi: unazungumziaje tuhuma zinazokukabili, je ni kweli kuwa ulichukua fedha kinyume na utaratibu.
Kilungi: Kata simu nitakupigia baada ya nusu saa.
Baada ya kupita muda huo, rais huyo hakupiga simu, hata alipopigiwa simu yake iliita tu bila majibu.
Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Uhusiano wa Chuo
hicho, Leonidas Tibanga aliliambia gazeti hili kwa kifupi kuwa uongozi
wa CBE hauwezi kushirikiana na wanafunzi kufanya udanganyifu wowote kwa
sababu fedha hizo ni zao na siyo za chuo
إرسال تعليق