MADAI: Sakata la Rais CBE lachukua sura mpya

Dar es Salaam. Sakata la Rais wa Serikali ya Wanafunzi ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dar es Salaam, Ramadhan Kilungi kudaiwa kughushi saini na kuiba Sh32 milioni katika akaunti ya Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho (Cobeso), limechukua sura mpya baada ya baadhi ya wanafunzi kudai kuwa utawala wa chuo hicho unahusika.
Habari kutoka ndani ya chuo hicho zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa kabla ya Kilungi kuchota fedha hizo Februari 7, mwaka huu, mwanzoni mwa Januari alichota tena Sh12 milioni katika akaunti hiyo kwa ajili ya safari ya Bunge la wanafunzi lililotembelea vikao vya Bunge mjini Dodoma.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kwa nyakati tofauti,  kuanzia Oktoba 2, mwaka jana hadi Januari 26 mwaka huu,  Bunge la wanafunzi limekuwa likiuandikia barua utawala wa chuo hicho kutaka ufafanuzi wa matumizi ya fedha na kushinikiza  vifanyike vikao, lakini utawala ulizuia.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki alisema kwa sasa Kilungi yuko nje kwa dhamana na uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili unaendelea.
“Kwa sasa yupo nje kwa dhamana na uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani,” alisema Nzuki.
Kilungi alipotafutwa na gazeti hili jana, mazungumzo yalikuwa hivi;
Mwananchi: Pole kwa matatizo yaliyokupata.
Kilungi: Asante.
Mwananchi: unazungumziaje tuhuma zinazokukabili, je ni kweli kuwa ulichukua fedha kinyume na utaratibu.
Kilungi: Kata simu nitakupigia baada ya nusu saa.
Baada ya kupita muda huo, rais huyo hakupiga simu, hata alipopigiwa simu yake iliita tu bila majibu.
Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Uhusiano wa Chuo hicho, Leonidas Tibanga aliliambia gazeti hili kwa kifupi kuwa uongozi wa CBE hauwezi kushirikiana na wanafunzi kufanya udanganyifu wowote kwa sababu fedha hizo ni zao na siyo za chuo

Post a Comment

Previous Post Next Post