Jordan yathibitisha kifo cha Rubani wake

Rubani wa Jordan Luten Moaz al-Kasasbeh wakati wa uhai wake
Jordan imethibitisha kifo cha rubani Moaz al-Kasasbeh baada ya picha ya video kuchapishwa katika mtandao na kikundi cha Islamic State, IS kilichodai kumwonyesha akichomwa moto angali hai.
Video hiyo inamwonyesha mtu akiwa amesimama katika kisanduku kilichozingirwa na moto. Maafisa wanafanya kazi ya kuthibitisha ukweli wa video hiyo.
Mfalme Abdullah wa Jordan, amempongeza Luteni Kasasbeh kama shujaa, akisema Jordan lazima "iungane" katika machungu.
Rubani huyo alikamatwa wakati ndege yake ilipotua karibu na mji wa Raqqa, nchini Syria, wakati wa operesheni ya kijeshi dhidi ya IS mwezi Desemba.
Picha hiyo ya video ilitumwa Jumanne na kusambazwa kupitia mtandao wa Twitter unaojulikana kama chanzo cha habari za propaganda za kikundi cha IS.
Video hiyo ya dakika 22 inamwonyesha rubani wa Jordan akipita katika maeneo ya vifusi huku akiwa ameelekezwa mtutu wa bunduki. Vifusi hivyo vimesababishwa na mashambulio ya anga ya majeshi washirika yakiwalenga wapiganaji wa Kiislam.
Mwandishi wa BBC wa masuala ya usalama Frank Gardner anasema dunia tayari imeshitushwa na vitendo vya kikatili vya Islamic State, huku video hiyo ya kuogofya ikiwalenga Waarabu nchini Jordan na mataifa ya Ghuba.
Televisheni ya serikali ya Jordan imeripoti kuwa Luteni Kasasbeh, mwenye umri wa miaka 26, aliuawa mwezi mmoja uliopita na tangu wakati huo jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika kutaka kumwokoa.
Nchi hiyo imeapa "adhabu na kulipiza kisasi" kwa kifo chake, na mfalme ameielezea IS kama"kundi katili la uhalifu".
- BBC

Post a Comment

Previous Post Next Post