Jordan
imethibitisha kifo cha rubani Moaz al-Kasasbeh baada ya picha ya video
kuchapishwa katika mtandao na kikundi cha Islamic State, IS kilichodai
kumwonyesha akichomwa moto angali hai.
Video hiyo inamwonyesha mtu
akiwa amesimama katika kisanduku kilichozingirwa na moto. Maafisa
wanafanya kazi ya kuthibitisha ukweli wa video hiyo.
Mfalme Abdullah wa Jordan, amempongeza Luteni Kasasbeh kama shujaa, akisema Jordan lazima "iungane" katika machungu.
Rubani
huyo alikamatwa wakati ndege yake ilipotua karibu na mji wa Raqqa,
nchini Syria, wakati wa operesheni ya kijeshi dhidi ya IS mwezi Desemba.
Picha
hiyo ya video ilitumwa Jumanne na kusambazwa kupitia mtandao wa Twitter
unaojulikana kama chanzo cha habari za propaganda za kikundi cha IS.
Video
hiyo ya dakika 22 inamwonyesha rubani wa Jordan akipita katika maeneo
ya vifusi huku akiwa ameelekezwa mtutu wa bunduki. Vifusi hivyo
vimesababishwa na mashambulio ya anga ya majeshi washirika yakiwalenga
wapiganaji wa Kiislam.
Mwandishi wa BBC wa masuala ya usalama
Frank Gardner anasema dunia tayari imeshitushwa na vitendo vya kikatili
vya Islamic State, huku video hiyo ya kuogofya ikiwalenga Waarabu nchini
Jordan na mataifa ya Ghuba.
Televisheni ya serikali ya Jordan
imeripoti kuwa Luteni Kasasbeh, mwenye umri wa miaka 26, aliuawa mwezi
mmoja uliopita na tangu wakati huo jitihada mbalimbali zimekuwa
zikifanyika kutaka kumwokoa.
Nchi hiyo imeapa "adhabu na kulipiza kisasi" kwa kifo chake, na mfalme ameielezea IS kama"kundi katili la uhalifu".
- BBC
إرسال تعليق