Kipindi cha kampeni za uchaguzi zinapokaribia, ni wakati muhimu
sana kwa wananchi kuongeza umakini katika kusikiliza na kuamua ipi ni
hoja au ahadi ya msingi kwa mustakbali wa nchi yetu.
Ni hatari kama Watanzania tutakubali kuzugwa na
hoja au ahadi za wagombea ambazo pengine kwa ufinyu wa upembuzi wetu,
tutabaki kuziona na kuzishangilia kama hoja au ahadi mwanana kwa
mustakbali wa nchi yetu, kumbe haziwezi kutusaidia kwenda mbele.
Ni ukweli usiopingika kuwa, nchi yetu inahitaji mageuzi makubwa hasa kwenye sekta ya elimu ili tusonge mbele kwa mafanikio.
Mwaka 2002 tulitangaziwa kuwa elimu ya msingi ni
bure. Serikali iliahidi kutoa ruzuku ya Sh10,000 kwa kila mwanafunzi
kuchukua nafasi ya mchango wa Upe. Ni kwa kiasi gani Serikali
imezingatia na kutimiza ahadi yake hii?
Ni kwa kiasi gani ruzuku ambayo imekuwa ikitolewa
imesaidia kuifanya elimu ya msingi kuwa ya bure? Je, ni kwa kiasi gani
ruzuku hii imemsaidia mzazi kupunguza gharama za kununua madaftari,
kalamu, vitabu, usafiri na michango mingine ya shule?
Yumkini ni wale tu wasioona wanaweza kuunga mkono
ghiliba hizi za kutaka kurudisha nyuma juhudi za wananchi kuboresha
huduma za shule zao kupitia michango yao ya hali na mali.
Je, ni kipi hasa kinachangia Taifa letu
kutoandikisha watoto wengi shule za sekondari? Ni karo, au gharama hizi
zinazobebwa na wazazi?
Tufute karo au tusaidie wazazi wasiojiweza kukidhi
mahitaji ya watoto wao shuleni? Hili linawezekana kwa kuweka utaratibu
maalumu wa wazazi kushiriki katika harakati za kutengeneza mazingira
rafiki ya kufundishia na kujifunzia?
Tujiulize hayaKuna mambo mengi tunatakiwa
tujiulize kabla ya kukimbilia kauli hizi za wanasiasa. Ni kwa kiasi gani
kwa mfano, kwa kuondoa karo kutasaidia kuongeza vitabu shuleni ikiwa
hata Sh25,000 zinazotakiwa kutolewa kwa kila mwanafunzi wa sekondari
hazifiki?
Je, kuondoa karo kutasaidiaje walimu kupata
mafunzo kazini, kupata vitendea kazi mfano chaki na madaftari ya
maandalio ambayo Serikali ilishasahau kutoa kwa miaka mingi?
Najua uamuzi wa kuifanya elimu ya sekondari kuwa
bure itafuatiwa na ahadi ya Serikali kutoa ruzuku kufidia pengo. Ahadi
za namna hii hazijaanza leo.
Kwa kiasi gani Serikali imetimiza ahadi zake kila
inapoanzisha mipango ya namna hii? Tumeshuhudia katika kipindi cha miaka
10 ya awamu ya kwanza na ya pili ya MMEM, hakuna hata mwaka mmoja
Serikali imeweza kupeleka shuleni hiyo fedha iliyoahidi.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق