Dar es Salaam. Kifungo cha miezi 12
walichopewa makada sita wa CCM kwa kukiuka kanuni na taratibu za chama
hicho na kuanza kampeni za kuwania urais kabla ya wakati, kinamalizika
ndani ya saa 24 na hatma yao kusubiri tathimini itakayofanywa na kamati
ndogo ya maadili ili kubaini iwapo walitekeleza ipasavyo adhabu hiyo au
la.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape
Nnauye alithibitisha jana kuwa muda wa adhabu hiyo unaelekea ukingoni
na kufafanua kuwa viongozi hao watafanyiwa tathmini na kamati ndogo ya
maadili ili kubaini kama walitekeleza ipasavyo adhabu hiyo.
Makada hao walipewa adhabu hiyo ya onyo kali na
Kamati Kuu Februari 18, mwaka jana baada ya kuthibitika kuanza kampeni
za kutafuta kuteuliwa kugombea urais kabla ya wakati kinyume na kanuni
za uongozi na maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i).
Vilevile baada ya kuhojiwa, walithibitika kufanya
vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na baadhi yao kufanya
vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii.
Kutokana na adhabu ya onyo kali makada hao kwa
mwaka mzima walikuwa katika hali ya kuchunguzwa ili kuwasaidia katika
jitihada za kujirekebisha.
Pia kamati ndogo ya udhibiti iliagizwa
kuwachunguza na kuchukua hatua kwa wote waliohusika kwa namna moja au
nyingine (mawakala na wapambe), kufanyika kwa vitendo hivyo vilivyovunja
kanuni za chama.
Makada hao waliokuwa chini ya adhabu hiyo ni
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick
Sumaye, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January
Makamba, Waziri wa Kilimo na Ushirika, Stephen Wasira na Mbunge wa
Sengerema, William Ngeleja.
Kwa nyakati tofauti jana, makada hao walizungumza
na gazeti hili na kueleza kuwa wanasubiri kauli ya chama hicho baada ya
adhabu yao kumalizika.
Kauli ya Nape
Akizungumza na gazeti hili jana Nape alisema,
“Kanuni zetu zipo wazi. Adhabu ikimalizika itafanyika tathmini ili
kubaini utekelezaji wa adhabu kwa wahusika.”
Hata hivyo, Nape alisema hakuna muda maalumu wa
kufanya tathmini hiyo na kusisitiza kuwa inaweza kufanywa kwa siku moja,
wiki au miezi, “Itategemea kazi yake itamaliza lini. Kamati ikimaliza
kazi yake itawasilisha ripoti katika vikao vya juu vya chama.”
Nape alisisitiza kuwa adhabu kwa viongozi hao
ilianza pale ambapo waliambiwa kuwa wamepewa adhabu, alipotakiwa kutaja
tarehe ambayo walianza adhabu hiyo alisema kuwa haikumbuki, ila ilikuwa
mwaka jana mwezi kama huu
إرسال تعليق