Tanga. Tukio la kurushiana risasi kati ya
polisi wakishirikiana na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
dhidi ya watu wanaosadikiwa kuwa majambazi au magaidi limeacha maswali
10 muhimu yanayolifanya lionekane lenye utata.
Mpaka sasa hakuna taarifa za kina juu ya tukio
hilo lililotokea siku nne zilizopita na kusababisha kifo cha mwanajeshi
na wapiganaji wengine zaidi ya sita ambao hawajajulikana kujeruhiwa.
Jana katika mkutano wake na waandishi wa habari
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Magalula Said Magalula alijaribu kujibu baadhi
ya maswali hayo ambayo yamewafanya wananchi wa Tanga na mikoa mingine
nchini, kupata taharuki na kufananisha tukio hilo na matukio ya kigaidi
yanayotokea katika nchi mbalimbali duniani.
Hata hivyo, majibu ya Magalula, kama ilivyokuwa
katika taarifa ya awali iliyotolewa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo
wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, yaliwaacha waandishi wa habari na
maswali mengi kuliko majibu, kwani mbali na kuwatoa hofu wananchi, kuna
maswali aliyajibu kwa kifupi bila ufafanuzi wa kutosha, hivyo kuzidi
kulifanya tukio hilo kuwa na utata.
Swali la kwanza ambalo wananchi wanajiuliza ni iwapo tukio hilo ni la kigaidi au ujambazi?
Akijibu swali hilo na kukataa kuulizwa swali la aina hiyo tena, Magalula alisema tukio hilo ni la ujambazi.
Kauli ya mkuu huyo wa mkoa inafanana na ya Waziri
wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mathias Chikawe ambaye juzi aliliambia gazeti
hili kuwa tukio hilo ni la uhalifu wa kawaida.
Alisema polisi wanafahamu kuwa kuna hali ya hatari
na wameshaongeza ulinzi katika maeneo yote, kwamba juhudi zaidi
zinaendelea kufanyika ili kulinda usalama wa raia na kuifanya Tanzania
ibaki kuwa kisiwa cha amani.
Swali la pili, waliohusika katika mashambulizi hayo ni raia wa nchi gani?
Magalula alisema swali hilo halina majibu na
kwamba majibu yake yatapatikana baada ya kukamatwa kwa watu hao
wanaosadikiwa kuwa ni majambazi.
Juzi, Kamishna Chagonja alikaririwa akisema
mapigano hayo yalifanyika katika msako wa majambazi walioiba silaha
kwenye kituo cha polisi mkoani Tanga, huku taarifa nyingine zikisema
mmoja wa watuhumiwa tayari alikuwa mikononi mwa polisi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi
Makosa ya Jinai nchini (DCI), Diwani Athumani alisema matukio ya uhalifu
yanayotokea nchini ni mapya na yanayochochewa na ukuaji wa teknolojia
ya habari na mawasiliano- Mwananchi
إرسال تعليق