Mkenya atua Simba SC, Matola out

UONGOZI wa Simba umelazimika kuachana na kocha msaidizi, Selemani Matola na tayari kuna taarifa kuwa nafasi yake itachukuliwa na Mkenya, Yusuf Chippo ambaye aliwahi kuifundisha Coastal Union ya Tanga.
Simba imefikia hatua hiyo baada ya kujadili kwa kina barua aliyoiandika Matola kwa viongozi wake kutaka kupumzika ili kutatua matatizo ya kifamilia lakini pia akiomba au kubadilishiwa majukumu.
Lakini chanzo cha kina kimeliambia Championi Jumatano kuwa tayari viongozi wamefikia maamuzi ya kuachana naye na nafasi yake itachukuliwa na Chippo ambaye kwa sasa ni kocha wa FC Leopards ya Kenya. Chippo aliwahi kuifundisha timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ kama kocha msaidizi.
“Uongozi umeamua kuachana naye (Matola) baada ya kujadili barua yake aliyoiandika hivi karibuni na tayari mikakati ya kupata mbadala wake imeanza na wako kwenye mazungumzo na yule kocha Mkenya Chippo aliyewahi kuifundisha Coastal,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, Championi Jumatano ilipomtafuta Rais wa Simba, Evans Aveva simu yake iliita bila kupokelewa licha ya kupigiwa mara kadhaa.
Simba imekuwa na mwendo wa ‘kobe’ misimu mitatu mfululizo licha ya kubadili makocha mara kwa mara, ambapo Matola aliteuliwa msimu uliopita kuchukua nafasi ya Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ baada ya mabadiliko ya benchi zima la ufundi kwa kuwaondoa Abdallah Kibadeni na Julio na nafasi zao kuchukuliwa na Mcroatia, Zdravko Logarusic na Matola katika mzunguko wa pili.
 Chippo amewahi kuzifundisha timu nyingine kama Ulinzi Stars ya Kenya na FC Leopards ya Kenya ambapo alipo sasa.
Wakati gazetini hili likijiandaa kwenda mitambo lilipata taarifa kuwa Matola amepelekwa kukinoa kikosi B hiyo ni kwa mujibu wa katibu wa timu hiyo, Stephen Ally.
Nicodemus Jonas, Khadija Mngwai na Martha Mboma

Post a Comment

Previous Post Next Post