Dar es Salaam. Kamati iliyoundwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG), kuchunguza mabilioni ya fedha yaliyofichwa na baadhi ya
Watanzania katika benki mbalimbali nchini Uswisi, imekamilisha uchunguzi
na inasubiri kukabidhi ripoti ya kazi hiyo kwa Spika wa Bunge.
Hayo yalisemwa jana na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, George Masaju alipokuwa akizungumza na wahariri wa vyombo
mbalimbali vya habari, Dar es Salaam.
Masaju alisema kamati hiyo ilikamilisha kazi yake
baada ya kuwahoji watu mbalimbali na kukamilisha kazi hiyo kama
walivyoagizwa na Bunge na kinachosubiriwa ni kuikabidhi kwa chombo hicho
cha kutunga sheria.
“Ofisi yangu kupitia kamati iliyoundwa
tulikwishamaliza kazi hii, lakini hatuwezi kutoa taarifa kupitia sehemu
nyingine zaidi ya ofisi iliyotupatia kazi kama utaratibu unavyoelekeza.
“Sasa wananchi na nyie waandishi wa habari msubiri
taarifa hiyo itolewe kule bungeni ambako tuhuma hizi zilianzia,”
alisema Masaju.
Watuhumiwa
Vigogo 10 wametajwa kuhusika katika kashfa hiyo.
Inadaiwa kuwa katika orodha hiyo, yupo kiongozi mmoja mwandamizi
mstaafu, maofisa watatu wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ), mawaziri wastaafu ambao baadhi yao bado ni wabunge na aliyewahi
kuwa kiongozi mwandamizi wa Benki Kuu Tanzania (BoT).
Kamati ilivyoundwa
Kamati hiyo maalumu iliundwa kwa Azimio la Bunge
baada ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kuibua tena tuhuma hizo
bungeni mapema mwaka jana, akidai kuna vigogo walioficha Sh323.4
bilioni katika benki mbalimbali za Uswisi.
Kiasi hicho cha fedha kinaweza kujenga barabara ya
lami yenye urefu wa kilomita 300 ambao ni sawa na kutoka Morogoro hadi
Iringa.
Kwa mara ya kwanza, tuhuma hizo zilitolewa bungeni
na Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), mwaka 2012.
Katika kikao cha Tisa cha Bunge, Zitto
aliwasilisha hoja binafsi kulitaka Bunge kuchunguza na kuielekeza
Serikali kuchukua hatua dhidi ya Watanzania aliowaita vigogo walioficha
fedha na mali haramu nje ya nchi.
إرسال تعليق