Shahidi wa nane katika kesi ya jinai inayomkabili
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa
Ponda (pichani), ameieleza Mahakama ya Hakimu mkazi mkoa wa Morogoro
namna alivyofanikiwa kurekodi mkanda wa video kwa siri kwa kutumia
kamera ndogo ambayo ilikuwa siyo rahisi kuonekana kwa watu.
Ameeleza mahakamani kuwa wakati akichukua mkanda huo wa video
alichukua taadhari kubwa huku akiwa amevalia nguo za kiraia baada ya
kutadharishwa na mkuu wake wa kazi kuwa tukio hilo linaweza kuhatarisha
maisha yake, hivyo ni muhimu kuwa na tahadhari kubwa wakati wa kurekodi
mkanda huo.
Shahidi huyo ambaye ni Askari polisi G1293 D/C Abdalah,
anayefanyakazi Ofisi ya Upelelezi mkoa wa Morogoro, alieleza mbele ya
Hakimu wa Mahakama hiyo, Mary Moyo, kuwa ilikuwa ni lazima kurekodi
Kongamano la Eid pili ambalo Sheikh Ponda alitoa maneno yenye kuumiza
imani za dini nyingine na pia alishawishi watu kutenda kosa.
Akiongozwa na Wakili Mkuu Mwandamizi wa Serikali, Benard Kongola,
alidai kuwa Agosti 10, 2013, jioni alipewa maelekezo na mkuu wake wa
kazi na kutakiwa kwenda kurekodi video kwenye kongamano hilo hivyo
alichukua kamera ndogo aina ya JVC ambayo haikuwa rahisi kuonekana kwa
watu.
Alisema alifika eneo la tukio na kuungana na waumini wengine kama
mmoja wa wasikilizaji wa kongamano hilo na kuanza kutoa kamera hiyo kwa
siri kisha kurekodi tukio hilo mpaka lilipomalizika bila kutambuliwa na
mtu yoyote katika eneo hilo.
Alidai kuwa kama alivyoelekezwa na mkuu wake wa kazi, baada ya
kumaliza kurekodi kongamano hilo alirudi ofisini akiwa na kamera hiyo
na kumkabidhi mkuu wake wa kazi.
Wakili wa Utetezi, Abubakari Salimu alimuuliza Shahidi huyo, kama
alitumwa kurekodi video katika kongamano hilo je, hakusikia mlio wa
bomu, na je, kamera na shahidi kipi kinaweza kutunza kumbukumbu.
Akijibu maswali hayo shahidi huyo alieleza kuwa kazi yake ilikuwa
ni kwenda kurekodi na siyo kusikiliza milio ya mabomu na kwamba yeye
siyo mtaalamu wa mabomu, hivyo hawezi kutofautisha mlio wa bomu na
gurudumu la gari likipasuka.
Kesi hiyo itaendelea Februari 26, mwaka huu
إرسال تعليق