Kopunovic sasa kiburi, aionya Yanga, straika

KOCHA wa Simba, Goran Kopunovic, alifanya uamuzi mgumu juzi Jumapili katika mchezo na Polisi Morogoro kwa kuamua kumweka benchi straika namba moja wa timu hiyo, Danny Sserunkuma na kumwanzisha Ibrahim Ajibu jambo ambalo anasema alikuwa sahihi kabisa.
Kocha huyo mwenye mbwembwe nyingi, alisema hawezi kumpanga mchezaji kwa kuangalia anatoka nchi gani ama alifanya nini katika mechi ya mwezi uliopita, bali anaangalia mahitaji ya timu kwa wakati huo na umakini wa mchezaji husika.
Uamuzi wa Kopunovic kumuweka benchi Sserunkuma umefanyika ikiwa ni wiki moja na nusu pekee tangu straika huyo alipoifungia Simba mabao yote mawili katika ushindi wa 2-1 dhidi ya JKT Ruvu.
Mserbia huyo aliongeza kuwa Sserunkuma anatakiwa kufunga kila mechi na si kushangilia mabao aliyofunga katika mechi zilizopita huku akisifu kiwango kilichoonyeshwa na Ajibu katika mechi yao hiyo ya juzi.
Ajibu na Elius Maguli walifunga bao moja kila mmoja na kuipatia Simba ushindi wa mabao 2-0 ugenini.
“Naangalia mafanikio ya timu zaidi na si mchezaji mmoja mmoja, nilichofanya ni kwa manufaa ya timu na nitaendelea kuwapanga wachezaji kutokana na uwezo na si eneo analotoka.
“Dan (Sserunkuma) alifanya makosa mengi katika mechi ya Coastal Union, alikosa nafasi tatu hadi nne za wazi hivyo nikalazimika kubadili mfumo na kumchezesha Ajibu,” alisema kocha huyo wa zamani wa Polisi Rwanda.
AZIONYA AZAM, YANGA
Baada ya kikosi chake kupaa hadi nafasi ya nne katika msimamo wa ligi na kupunguza wigo wa pointi na vinara wa ligi Azam na Yanga kutoka pointi nane hadi tano, Kopunovic amezitahadharisha timu hizo kuwa zikae chonjo kwani anakuja.
Alisema bado ana mechi dhidi ya Azam na Yanga ambazo kama akishinda ataweza kupunguza wigo huo na kuwakaribia kabisa wapinzani wake hao.
“Bado tuna nafasi, wigo wa pointi kati yetu, Azam na Yanga si mpana sana, kumbuka bado ligi imebakisha mechi 12 na kati ya hizo zipo ambazo tutacheza nao, ni lazima tushinde mechi hizo ili kuwakaribia ama kuwafikia,” alisema Kopunovic mwenye umri wa miaka 48.
IVO KUREJEA UWANJANI JUMATANO

Post a Comment

أحدث أقدم