Jeshi la Polisi limekamata bunduki ya SMG yenye
namba 14301230, risasi 20 na magazini moja mali ya polisi Tanga
vilivyokuwa imefukiwa ardhini kwenye pango walilokuwa wamejificha watu
wanadaiwa kuwa ni majambazi huku katika eneo la Amboni, jijini hapa.
Silaha hiyo ni miongoni mwa silaha mbili za SMG ambazo walidaiwa
kuporwa askari polisi wawili waliokuwa doria hivi karibuni jijini Tanga
na watu wasiojulikana.
Polisi pia wanamshikilia mtu mmoja (jina limehifadhiwa) anayedaiwa
kuhusika katika tukio hilo la uhalifu katika Kitongoji cha Kona Z,
Amboni.
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul
Chagonja, (pichani) alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi pamoja na
silaha hizo kupatikana siku hiyo kwa nyakati tofauti jijini Tanga.
Changonja alisema kukamatwa kwa mtu huyo kulitokana na ushirikiano
wa raia wema kwa Polisi ambaye baada ya kukamatwa kwake katika mahojiano
aliwapeleka askari hadi ndani ya pango walipokuwa wameficha silaha
hiyo.
“Katika eneo la kona Z ndipo tulipomkamata mtu huyo ambaye kwa
sababu za kiusalama hatuwezi kulitaja jina lake na baada ya mahojiano
marefu na polisi, alikubali kutupeleka walipokuwa wameficha silaha hii
moja ambayo ni miongoni mwa ile iliyoibwa kwa polisi wakiwa doria,”
alisema.
Kuhusu harufu za miili ya binadamu inayodaiwa kutoka ndani ya pango
hilo, alisema ni harufu ya ngedere ambao walikufa muda mrefu ndani ya
pango hilo.
“Hakuna mwili wa binadamu huko ndani ni ngedere ambao walikufa
ndani ya pango na walijeruhiwa …lile pango linaingiza kila aina ya
mnyama,” alisema Chagonja.
Alisema polisi wanaendelea na msako wa kuipata bunduki nyingine aina ya SMG na risasi 40 walizoporwa askari waliokuwa doria.
“Nasisitiza kwamba wananchi wawe na utulivu wakati tukiendelea na
operesheni ya kuwapata hawa wahalifu kwa sasa hatutataja idadi yao,
lakini wajue kuwa tumewatia nguvuni tayari…na waendelee kutupa
ushirikiano hasa pale wanapomwona mtu ambaye wanamtilia mashaka,”
alisema.
Hivi karibuni Askari Polisi wawili wakiwa katika doria waliporwa
SMG mbili zikiwa na risasi 60 na watu wasiojulikana jijini hapa.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment