Tahadhari kwa wanawake kwa mtu huyu!

Pichani Malaria akiwa amejipumzisha kwenye kibaraza cha maeneo ya ofisi za Idara ya Habari Maelezo kama alivyokutwa na mpiga picha wetu.
Na Andrew Chale, modewjiblog
Hali ya sintofahamu juu ya mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la ‘Malaria’,  imezidi kuwa kero kwa baadhi ya watu ikiwemo wanawake kwa mtu huyo kuwafanyia vitendo vya kidhalilishaji  kwa kuwashika sehemu  nyeti, na baada ya hapo kukimbia ama humtisha kwa lengo la kutaka kumpiga aliyemfanyia kitendo hicho.
Kwa siku kadhaa, modewjiblog imekuwa ikifuatilia mienendo ya mtu huyo ambaye pia inasemekana  kuna wakati huwa anarukwa na akili hali iliyopelekea kuitwa jina hilo la Malaria.
Baadhi ya watu walioongea na modewjiblog walieleza kuwa,  Malaria amekuwa kero kubwa kwa wanawake na wasichana hasa wanaopita usawa wa  ukumbi wa Idara habari MAELEZO na maeneo jirani ambapo huwanyatia na kisha kuwafanyia vitendo vya kidhalilishaji na kisha kukimbia.
Salum Ally ambaye ni Dereva Taxi, eneo hilo la MAELEZO, alibainisha kuwa, mtu huyo amekuwa akipigwa mara kwa mara na hata kupelekwa Polisi, lakini baada ya siku kadhaa anarejea maeneo hayo.
“Huyu mtu amekuwa kero sana hasa  kwa vitendo vyake vya kuwashika makalio wanawake pamoja na maziwa. Imekuwa hofu kubwa sana lakini mamlaka husika wanashindwa kuchukua hatua za haraka” alibainisha Salum.
DSCN9811
Malaria akiomba msaada wa hela kwa mmoja wa wanawake waliokua wamesimama karibu na maeneo ya ofisi za Habari Maelezo katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Monica Dorcas ambaye anafanya shughuli zake za kuuza vocha alibainisha kuwa,  kwa sasa Malaria ameibua hofu kubwa kwani, wakati mwingine humvizia mwanamke hata kama amemuona mbali na kisha kumfanyia vitendo hivyo.
“Kwa sasa akiona pia mwanamke amevaa nguo za kubana ama ana maumbile makubwa  kama amemuona toka mbali ama amempitia karibu yake, humfuata nyuma nyuma na kisha humshika makalio na kukimbia” alisema Monica.
pia tulishuhudia vitendo hivyo vya kudhalilisha wanawake hao, ambapo endapo ataona  anashindwa kutimiza adhma yake hiyo, Malaria hujifanya anamsalimia ama kumuomba msaada wa pesa ama kumuongelesha na  kisha  mwanamke ama msichana akijisahau humshika maziwa ama makalio na kukimbia.
Aidha, imebainika kuwa, mbali na kufanya vitendo hivyo, pia Malaria anatembea na sindano ama pini zenye ncha kali, ambapo huvizia wanawake  na kuwachoma. Ambapo inadaiwa kuwa mwaka jana aliwahi kutenda tukio la kumchoma mwanadada mmoja sindano, hali iliyopelekea kupigwa na kuwekwa ndani, lakini baadae walishangaa amerejea tena, ambapo yupo akirandaranda katikati ya jiji hasa maeneo hayo ya MAELEZO.
Tunatoa wito kwa mamlaka husika kuchukua hatua za haraka juu ya mtu huyu, kabla  ya matatizo zaidi hayajatokea kwa sasa kwani amezidi kuwa kero kwa watu wote.

Post a Comment

Previous Post Next Post