Tatizo la mimba kutungwa nje ya mfuko wa uzazi

Mimba kutunga nje ya mfuko wa uzazi ni tatizo ambalo linaweza kumpata mwanamke yeyote na linapaswa kufahamika mapema ili hatua muafaka zichukuliwe.
Kwa kawaida mimba hutunga ndani ya mfuko wa kizazi isipokuwa mara chache huweza kutokea nje ya eneo hili maalumu.
Katika nyumba ya uzazi kuna mirija inayoitwa fallopian ambayo kazi yake ni kusafirisha mayai kutoka katika kiwanda chake cha uzalishaji; ovari  hadi kwenye mfuko wa uzazi. Hapo ndipo mimba inapaswa kutokea.
Kwa bahati mbaya ama kutokana na hitilafu fulani mimba hiyo inaweza ikatungishiwa kwenye moja ya mirija miwili ya kizazi; upande wa kulia au kushoto.
Ikitokea hivyo, basi itafahamika kuwa mimba hiyo imetungwa nje ya kizazi. Vilevile mimba inaweza ikawa imetungwa nje ya nyumba ya uzazi au mirija.  Asilimia 95 ya mimba zinazotungwa nje ya uterasi ama nyumba ya uzazi hutokea  kwenye mirija hii ya fallopian. 
Mimba zinazotungwa kwenye fallopian husababisha misuli inayozunguka mirija hiyo kushindwa kufanya kazi kutokana na mgandamizo wa mimba inavyokua. Hii husababisha mishipa inayopita karibu na fallopian kupasuka na damu kutoka kwa wingi hali ambayo isiposhughulikiwa mapema inasababisha madhara zaidi na hata kifo kwa mama.
Chanzo cha tatizo
Chanzo cha bado hakijajulikana, hata hivyo kuna vihatarishi ambavyo humfanya mwanamke kuwa katika mazingira ya kupata tatizo hili,.
Viashiria hivyo ni pamoja na magonjwa kama maambukizi katika mfumo wa uzazi hasa yale yanayosababisha uvimbe.
Vihatarishi vingine ni kama vile matumizi ya vitanzi vya kuzuia mimba au kuoteana  kwa tishu za kwenye nyumba ya uzazi.
Mambo mengine yanayoweza kusababisha mimba kutungwa nje ya nyumba ya uzazi ni uvutaji wa sigara. Nikotini iliyoko ndani ya tumbaku huchochea kusinyaa kwa mirija ya ya fallopian na hata kusababisha mirija hiyo kuziba.
Jambo jingine ni upasuaji wa tumbo uliofanyika zamani unaohusu mirija ya fallopian na kusababisha mrija husika kusinyaa.

Post a Comment

أحدث أقدم