UPANDE
 wa Mashikata kesi inayomkabili Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za 
Kiislamu nchini, Shehe Ponda Issa Ponda umewasilisha ushahidi muhimu wa 
mkanda wa video unaodaiwa kuonesha uhalisia wa tukio zima la kesi yake 
inayomkabili ya kutoa maneno ya uchochezi.
  
  
  
  
  
  
  
  
  
  
  
  
  
  
  
  
Mkanda
 huo wa video uliletwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkoa wa 
Morogoro, Mary Moyo na kuoneshwa na shahidi wa tano wa kesi hiyo ambaye 
ni askari kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi kitengo maalumu cha 
uchunguzi wa picha, Aristides alieleza vigezo alivyovitumia kuitambua 
uhalisia wa video hiyo iliyochukuliwa Agosti 10 mwaka 2013.
Shahidi
 huyo akiongozwa na Wakili wa Serikali, Benard Kongola alieleza 
mahakamani hapo kuwa video aliichunguza na kugundua kuwa ilichukuliwa 
katika eneo la tukio kupitia kamera ndogo aina ya JVC na kwamba baada ya
 kuichunguza aliandika hati na taarifa iliyoeleza vigezo alivyovitumia 
katika uchunguzi huo na yale aliyoyaona na kuyasikia katika video hiyo 
ambayo aliitoa mahakamani kama kielelezo.
  
Pamoja
 na ushahidi wake, lakini pia aliionesha video hiyo mahakamani hapo 
ambapo ilionesha tukio zima pamoja na maneno aliyoyatoa Shehe Ponda 
ambayo yanadaiwa kuwa yalikuwa ya uchochezi na yaliyoumiza imani ya dini
 nyingine.
Shahidi huyo pia alitoa kamera, DVD, hati na taarifa ya uchunguzi wa video hiyo kama kielelezo na kupokewa na mahakama hiyo.
Aliyekuwa
 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna msaidizi wa Polisi, 
Faustine Shilogile alikuwa shahidi wa nne katika kesi hiyo ambaye 
alieleza kuwa baada ya kupata taarifa za kutafutwa kwa Shehe Ponda 
kufuatia tuhuma mbalimbali zilizomkabili yeye kama kiongozi wa jeshi la 
polisi mkoa aliandaa askari kwa ajili ya kumkamata baada ya kufika 
mkoani Morogoro.
Shahidi
 huyo alidai kuwa taarifa hizo za kiintelijensia zilimhusisha Ponda na 
tuhuma za kumwagia tindikali wasichana wawili raia wa Uingereza huko 
Zanzibar na tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi jijini Dar es Salaam na 
kwamba tuhuma hizo alizipata wakati akiwa kwenye adhabu ya kifungo cha 
nje cha mwaka mmoja ambapo pia alitakiwa kutofanya kosa lolote katika 
kipindi hicho cha mwaka mmoja.
Upande
 wa utetezi ukiongozwa na wakili Juma Nasoro ulimuuliza maswali shahidi 
huyo, hata hivyo baadhi ya watu waliokuwepo mahakamani hapo walishindwa 
kuzuia vicheko vyao kutokana na aina ya maswali yaliyokuwa yakiulizwa 
pamoja na majibu yaliyokuwa yakitolewa.
Wakili wa utetezi: “Je wewe ulijuaje kama Shehe Ponda alitoa maneno ya uchochezi?”
Shahidi: “Niliambiwa na OCD wangu kupitia radio call (simu ya upepo) kwani alikuwepo eneo la tukio.”
Wakili: “Je, unayajua mashitaka yanayomkabili Shehe Ponda?”
Shahidi: ”Siyafahamu kwa kuwa mimi sio muandaaji wa hati ya mashitaka.”
Wakili: “Ni askari wangapi uliwaandaa kumkamata Shehe Ponda?”
Shahidi: “Sikumbuki”
Wakili: “Je, hukuandaa askari 25 hadi 30 kwa ajili ya kumkamata Shehe Ponda? “
Shahidi: “Wewe ndio utakuwa umeeleza hiyo idadi”
Wakili: ”Je, askari wako walikuwa na silaha na kama walikuwa nazo tunaweza kuamini kuwa wao ndio waliomjeruhi Shehe Ponda?”
 Shahidi: “Ndiyo baadhi ya askari wangu walikuwa na silaha lakini siwezi kufahamu Shehe Ponda alijeruhiwa na nini.”
Wakili: “Je, unajua kama Msemaji wa Polisi, Advera Senso alitoa taarifa kuwa kuna askari alisimamishwa kazi kupisha uchunguzi?” 
Shahidi: “Sina taarifa na kama alitoa taarifa hizo basi ni yeye na sio mimi.”
Wakili: “Je, kibali cha kufanya kongamano kilitolewa na nani na je uliambiwa kama Shehe Ponda ni mzungumzaji katika kongamano hilo?”
Shahidi: “Kibali kilitolewa kwa OCD na sikuwa na taarifa kama Shehe Ponda atakuwa mzungumzaji.”
Awali,
 upande wa mashtaka ulipanga kusikiliza mashahidi watano hata hivyo 
mahakama ilishindwa kuendelea kusikiliza mashahidi wengine watatu 
kutokana na muda kuwa umekwisha hivyo mashahidi hao watatu wataendelea 
kusikilizwa leo Februari 10 katika mahakama hiyo.
Hata
 hivyo, kesi imeendelea kuvuta hisia za wakazi wengi wa mkoa wa Morogoro
 na maeneo mengine huku hali ya ulinzi katika viwanja vya mahakama hiyo 
ikiwa imaimarishwa na kufikia hatua ya kuweka vifaa maalumu vya 
kuwakagua watu wanaoingia katika mahakama hiyo.

Post a Comment