Hatimaye klabu ya Yanga imekubali kulipa deni analodaiwa mchezaji wao,
Mrisho Ngassa na klabu ya Simba, kwa masharti iwapo tu atakubaliana nao
katika baadhi ya mambo likiwamo la mkataba au jambo lingine lolote.
Aidha, Ngassa ameahidi kucheza kwa kiwango katika michuano ya ligi na ya
kimataifa na kuwa mchezaji bora iwapo tu uongozi wa klabu hiyo
utamsaidia kulipa deni hilo kama ulivyoahidi.
Katika msimu wa 2013/2014, Ngassa alijiunga na Yanga akitokea Simba
alikokuwa akicheza kwa mkopo akiwa ni mali ya Azam FC, katika uhamisho
ambao Shirikisho la Soka Tanzania (TF), lilimuamuru awalipe Simba Sh
milioni 30 walizomsajili kutoka Azam FC na Sh milioni 15 kama fidia
baada ya kugundulika alisajiliwa timu mbili.
Kutokana na Yanga kuonesha nia ya kutaka huduma ya winga huyo, klabu
hiyo chini ya Mwenyekiti Yussuf Manji uliamua kumlipia deni hilo kwa
makubaliano atakuwa akikatwa Sh 500,000 katika kila mshahara wake wa
mwezi.
Hivi karibuni, Ngassa alisema alishindwa kucheza kwa kiwango cha juu
kutokana na kukatwa mshahara wake wote kwa ajili ya deni hilo katika
benki kinyume cha makubaliano yake na Yanga aliyodai walimuahidi
kumsaidia kulilipa.
Akitolea ufafanuzi suala hilo jana Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha
Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro alisema wamepata ombi la
Ngassa kuwa anaomba kulipiwa deni hilo na wamelipokea na kuahidi
kumsaidia ndani ya wiki moja, lakini awe tayari kutimiza masharti
atakayopewa bila kuyataja ni yapi.
“Ngassa ni mchezaji wetu tutamsaidia kulipa deni kwa sababu bado
tunamhitaji na yeye anatuhitaji,” alisema Murro na kuongeza kuwa
mchezaji huyo alikuwa akikatwa mshahara wote kwa sababu alikiuka
utaratibu waliowekeana na benki hiyo ambapo awali walikubaliana mshahara
wake uwe unapitia benki.
Alisema wakati Ngassa anakopa fedha, Yanga ilisimama kama mdhamini tu na
wakakubaliana mshahara wake uwe unapita benkiili awe anakatwa Sh
500,000, lakini baadaye akawa hafanyi hivyo kwani alikuwa akienda
kuchukua mshahara wake chini ya aliyekuwa Katibu Mkuu Beno Njovu bila
kupitisha huko kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Alisema kitendo hicho kilisababisha benki hiyo kulalamika kwa barua kwa
kukiuka makubaliano ya awali na ndipo uongozi mpya chini ya Katibu Mkuu
Dk Jonas Tiboroha, ulipoamua kupitisha mshahara huo benki ili akatwe
kama walivyokubaliana awali.
“Benki walikuwa na hasira kwa kutopata pesa zao kwa kipindi cha mwaka
mmoja na ndio maana walikuwa wakikata kwa hasira mshahara wote wa
Ngassa, sisi tulipoingia tukaona tufuate sheria kwani deni lile halikuwa
la kiuongozi,” alifafanua Murro.
Alisema wao kama klabu hawana matatizo ya kimaslahi kwani kazi yao kubwa
ni kutimiza majukumu ya mkataba na kwamba wanatambua kuwa Ngassa ni
mchezaji wao, ana uhuru wa kuzungumza mambo yake, lakini sio klabu.
Kuhusu kumuongezea mkataba, alisema watafanya mazungumzo na mchezaji
huyo kuona kama atasaini mkataba mpya kwa vile bado wanahitaji huduma
yake, lakini ikiwa hatakubali na atataka kuondoka, itakuwa sawa.
Hata hivyo, Ngassa ambaye alikuwepo kutolea ufafanuzi madai yake,
alisema anapenda kuendelea kuichezea Yanga ili kujenga heshima yake na
kama basi, ataondoka sio kucheza katika timu za ndani labda nje ya
Tanzania.
Pia, kuhusu kitendo chake cha kuwaomba msamaha mashabiki wa Simba na
Azam FC kwa kujutia kujiunga na Yanga, alisema sio kwamba ameisaliti
timu yake kwani hana mpango wa kurudi huko wakati huo akiwaomba msamaha
mashabiki wa Yanga kwa kitendo hicho.
Kuhusu kujutia kutokwenda El Merreikh, alisema ni kweli alikataa
kujiunga na timu hiyo kwa sababu ya mapenzi yake makubwa ilikuwa ni
kuichezea Yanga na hata sasa anapenda kuendelea kuichezea timu yake
hiyo.
إرسال تعليق