Mnikulu, Shaban Gurumo.
Pia ametaka watu wote, wakiwamo wabunge na baadhi ya vyombo vya 
habari waliohusika kutangaza kwamba, alipokea Sh. milioni 800 kutoka kwa
 Rugemalira wakati siyo kweli, wachukuliwe hatua kama zilizochukuliwa 
dhidi yake, ikiwamo kuhojiwa na kufikishwa mbele ya Baraza la Maadili ya
 Viongozi wa Umma, kujieleza kuhusiana na hilo. 
Alisema hayo wakati akiongozwa na wakili wake, Lucas Kamanija, 
kujieleza kuhusiana na malalamiko dhidi yake, yaliyowasilishwa na 
wanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma mbele ya 
baraza hilo, jijini Dar es Salaam jana.
Gurumo alidai Rugemalira ni rafiki yake takriban miaka 10 sasa, 
ndiye aliyemshauri kufungua akaunti kwenye Benki ya Biashara ya 
Mkombozi, tawi la St. Joseph, jijini Dar es Salaam, kabla ya kumuingizia
 Sh. 80, 850,000 katika akaunti hiyo.
Alidai aliyemuunganisha na Rugemalira, ni Dk. Fred Limbanga wa 
hospitali binafsi ya Sanitas, iliyoko Mikocheni, Dar es Salaam, ambaye 
jana alifika katika baraza hilo kutoa ushahidi upande wa utetezi.
AMSHANGAA RUGEMALIRA 
Hata hivyo, Gurumo aliliambia baraza hilo linaloongozwa na 
Mwenyekiti wake, Jaji Hamisi Msumi, kuwa hakutambua kusudio la 
Rugemalira kumuwekea fedha hizo kwenye akaunti hiyo.
Alidai anahisi pengine Rugemalira alifanya hivyo kwa kuwa kipindi 
hicho alikuwa ana mgonjwa anayesumbuliwa na maradhi ya saratani.
Hata hivyo, alidai hakujishughulisha kabisa kuuliza ili kujua sababu za Rugemalira kumuwekea fedha hizo kwenye akaunti yake.
Alidai aliitwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili 
kuhojiwa na kutakiwa kwenda na nakala ya taarifa ya benki hiyo, ambayo 
aliitambua jana mbele ya baraza hilo.
Hata hivyo, alidai yeye na Rugemalira hawajawahi kuzungumzia lolote
 kama fedha hizo ziliwekwa kwenye akaunti hiyo na kampuni ya VIP 
Engineering and Marketing Limited, kama hati ya malalamiko ilivyoeleza.
Alidai anafahamu kuwa kila mwaka mtumishi wa umma anatakiwa kutamka
 kwenye fomu maalumu ya ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa 
Umma kuhusu mali na madeni anayomiliki.
Kutokana na hali hiyo, alidai kila mwaka Sekretarieti ya Maadili ya
 Viongozi wa Umma imekuwa ikimwandikia barua kumtaka afanye hivyo na 
kwamba, mara ya mwisho aliyoandikiwa ilikuwa Oktoba 2, mwaka jana.
Alidai aliwahi kuwasilisha fomu kama hiyo kwenye Sekretarieti ya 
Maadili ya Viongozi wa Umma Septemba 29, ambayo ilipokelewa siku hiyo 
hiyo na kwamba, tarehe ya mwisho kuwasilisha tamko kwenye sekretarieti 
hiyo ilikuwa Desemba 31, mwaka jana.
Gurumo alidai hajawahi kutumia cheo chake kupata manufaa kutoka kwa
 mtu yeyote na pia haijawahi kuingia akilini mwake kuifikiria kampuni ya
 VIP Engineering and Marketing Limited.
Pia alidai hajawahi kuwa na uhusiano na Rugemalira wa kiuchumi wala wa kibiashara.
BUNGE, VYOMBO VYA HABARI
Alidai tuhuma kwamba, alipokea Sh. milioni 800 kutoka kwa 
Rugemalira, kwa mara ya kwanza alizisikia redioni zikizungumzwa na 
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, bungeni, akiwa ndani
 ya gari akitokea nchini Afrika Kusini.
Alidai baadaye tuhuma hizo zilichapishwa kwenye baadhi ya magazeti na katika mitandao ya kijamii.
“Awali, lilipokuja kwenye Sekretarieti (ya Maadili ya Viongozi wa 
Umma), cha kwanza lilikuwa ni Bunge na vyombo vya habari. Kwa sababu 
hiyo, kama inaruhusiwa, wahusika wachunguzwe nao wapitie kwenye mikondo 
hii hii, ambayo mimi napitia,” alisema Gurumo.
Alidai hata siku moja hajawahi kuwa na maslahi ya kiuchumi na 
Rugemalira, mbali na ya kifedha na pia hana uhusiano wowote na kampuni 
ya VIP Engineering and Marketing.
Hata hivyo, akihojiwa na Wakili wa Sekretarieti ya Maadili ya 
Viongozi wa Umma, Getrude Cyriacus, Gurumo alikiri kuwa Rugemalira ni 
mmiliki wa VIP Engineering and Marketing Limited.
ADAI KUWA ANA FEDHA NYINGI
Pia alikiri kuwa taarifa ya benki iliyotolewa ikionyesha 
aliingiziwa fedha hizo na VIP Engineering and Marketing iliyowasilishwa 
katika baraza hilo na shahidi wa upande wa malalamiko, Basilio 
Mwanakatwe jana kama kielelezo, ndiyo aliyoipeleka kwenye kamati ya 
uchunguzi ya sekretarieti hiyo ilipomhoji.
Vilevile, akihojiwa na wakili huyo, Gurumo alikiri kutumia fedha alizopewa na Rugemalira kwa matumizi yake binafsi.
“Ningeweza kufanya hivyo bila kutumia fedha hizo (alizopewa na 
Rugemalira). Nina fedha zaidi ya hizo za Rugemalira,” alitamba Gurumo 
mbele ya baraza hilo jana.
Alidai kila mfuko wa suruali aliyovaa umesheheni fedha, hivyo daima
 maishani mwake hapatwi na ukata kiasi cha kutegemea fedha za 
Rugemalira.
“Hapa nina fedha na huku nina fedha,” alisema Gurumo mbele ya 
baraza hilo, huku akijipigapiga kwenye mifuko ya suruali aliyovaa jana.
Hata hivyo, alikana fedha alizopewa na Rugemalira kuwa zilikuwa ni 
zawadi na pia alipotakiwa na Wakili Getrude kueleza kama zilikuwa ni 
mshahara au posho aliyolipwa na VIP Engineering and Marketing Limited na
 siyo zawadi, Gurumo alisisitiza kuwa hajui.
ADAI HAKUJUA FEDHA ZA NINI
Pia alipotakiwa na Wakili Getrude kueleza kama aliwahi japo tu 
kujiuliza sababu ya kupewa fedha hizo, Gurumo alisema hakuwa nayo na 
kwamba, tafsiri ya zawadi katika fedha alizopewa na Rugemalira haipo.
Akijibu swali la wakili mwingine wa upande wa malalamiko, Hassan 
Mayunga, Gurumo alidai pia kuwa hakujua kama fedha hizo ni zawadi au 
manufaa.
Pia akiongozwa na Wakili Kamanija, Gurumo alidai siyo sekretarieti 
hiyo tu, bali hata afisa ma-suul wake, ambaye ni Katibu Mkuu Ofisi ya 
Rais hana uwezo wa kumpangia matumizi ya fedha na kwamba, Rugemalira 
hajampa utaratibu wowote wa kutumia fedha alizompa.
Awali, shahidi wa upande wa malalamiko, Mwanakatwe, ambaye ni Afisa
 Uchunguzi, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, 
akiongozwa na Wakili Mayunga, alidai alikutana na Gurumo Desemba 19, 
mwaka jana wakati wa uchunguzi walioufanya dhidi yake kutokana na 
taarifa walizozipata kutoka vyanzo mbalimbali, ikiwamo vyombo vya habari
 na mitandao ya kijamii.
Alidai katika uchunguzi huo, walibaini kuwa Februari 5, mwaka jana,
 Gurumo alipokea kiasi hicho cha fedha kupitia tawi la benki hiyo na 
kwamba, katika mahojiano, alikiri kupokea fedha hizo.
Kutokana na hali hiyo, alidai kuwa Gurumo alikiuka sheria ya 
maadili ya viongozi wa umma inayokataza kiongozi wa serikali kupokea 
zawadi zaidi ya awadi ndogondogo na ukarimu wa kawaida, pia inakataza 
kiongozi wa umma kudai, kuomba au kupokea maslahi ya kiuchumi zaidi ya 
ukarimu wa kawaida au zawadi ndogondogo.
Alidai kamati ya uchunguzi pia ilibaini kuwa Gurumo hakutamka 
zawadi aliyopokea wala thamani yake na hakuikabidhi kwa afisa mas-uul 
wake ili amwambie matumizi yake na namna ya kushughulika nayo.
Shahidi huyo alidai pia kuwa kamati ilibaini kuwapo na mgongano wa 
maslahi na kwamba, Gurumo kwa nafasi aliyonayo serikalini, anafahamu 
siri nyingi, hivyo kitendo chake cha kupokea kwa mfanyabishara, ni 
dhahiri kuwa hakupanga mambo yake namna ambayo ingemzuia kujiingiza 
kwenye mgongano wa kimaslahi.
“Viongozi wa umma ndiyo injini ya uendeshaji, wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa viwango, wanapaswa kuonyesha mfano. 
Ukiukwaji wa maadili unaweza kuwakosha wananchi imani na serikali yao,” alidai shahidi huyo.
Hata hivyo, akihojiwa na Wakili Kama shahidi huyo alidai kuwa 
taarifa kwamba, Gurumo alipokea Sh. milioni 800 kutoka kwa Rugemalira, 
hazina ukweli na ndiyo alihojiwa na kamati ya uchunguzi ya sekretarieti 
kwa kuwa hawana utaratibu wa kupokea na ‘kumeza’ porojo. 
Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji Msumi alizipa pande mbili za shauri
 hilo muda hadi Machi 13, mwaka huu, wa kuwasilisha kwa maandishi 
maelezo yake ya mwisho kabla ya kuandaa maamuzi na kuyapeleka kwa 
mamlaka husika za nidhamu dhidi ya mlalamikiwa.
Leo baraza hilo linatarajia kusikiliza malalamiko dhidi ya Mtendaji
 Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Philip Saliboko,
 anayetuhumiwa kupokea Sh. milioni 40.4 katika mgawo wa fedha 
zilizochotwa katika akaunti ya Tegeta Escrow.
     CHANZO:
     NIPASHE
    

  Atamba ana fedha kuliko mamilioni aliyogawiwa, Adai hajui ni za nini ingawa alizifungulia akaunti
إرسال تعليق