Mwili wa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Marwa Omtima ukizikwa.
IGENGA MTATIRO, TARIME
MKAZI wa Kitongoji cha Nyaiheta, Kijiji cha Kewanja
Kata ya Kemambo wilayani Tarime, Mara, Marwa Omtima (55) ambaye ni kada
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ameuawa kwa kupigwa
mshale tumboni na mtu aliyetajwa kwa jina la Gamaina, mkazi wa kitongoji
hicho kulipotokea ugomvi usiku wa Machi 5, mwaka huu.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Tarime na Rorya limethibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kusema siku ya tukio, marehemu alipigwa mshale
majira ya usiku na kufariki dunia.
Mwili wa Marwa ukiagwa.
Jeshi hilo lilisema linaendelea kumsaka mtu aliyefanya mauaji hayo
ili kumkamata na kumfikisha mahakamani kujibu tuhuma zake za kuua huku
chanzo kilidaiwa ni ugomvi binafsi uliotokana na chuki za siku
zilizopita.
Ilielezwa kuwa, marehemu alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu
kwenye Hospitali ya Wilaya ya Tarime baada ya kuvuja damu nyingi.Katika
mazishi yaliyofanyika Machi 7, mwaka huu, msemaji wa familia hiyo ambaye
ni kaka wa marehemu Omtima, Masanda Omtima, aliwaambia waombolezaji
kuwa, familia haitakuwa na kisasi na familia ya mtuhumiwa.
Aliwaomba wanafamilia wa pande zote kuendelea kutembeleana kama
zamani huku akisema ni dhambi kuua mtu kwani aliye na mamlaka ya kuondoa
uhai wa binadamu ni Mungu.Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa Kituo cha
Polisi Nyamwaga aliyehudhuria mazishi hayo, OCD Simon Marwa Maigwa
alisema atahakikisha muuaji huyo anasakwa mahali popote alipokimbilia na
kutiwa nguvuni.
Miongoni mwa waombelezaji wa msiba huo walioshindwa kutoa ujumbe wao
kwa simanzi ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Esther Nicholas
Matiko aliyesema tukio hilo limetia aibu na kuichafua Mara.
Mazishi hayo yaliyovuta hisia za watu wengi kutoka vyama vya siasa na
viongozi wake, jamii na askari polisi kwani aliyeuawa kaka yake ni
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewanja Tanzania, Omtima (Chadema).
إرسال تعليق