KAULI ZA KEJELI NA KUUDHI ZA VIONGOZI KWA WANANCHI ZAWAKERA LHRC,SOMA WALICHOKISEMA LEO

 Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Dk. Helen Kijo-Bisimba, wakati akitoa taarifa juu ya mwenendo na hatua za kisheria kwa viongozi wa umma wanaokiuka maadili.Katikati ni Mkurugenzi wa Ujengaji Uwezo na Uwajibikaji wa LHRC, Imelda Urrio na kulia ni Ofisa Programu Dawati la Waangalizi Watendaji wa Serikali wa LHRC, Hussein Sengu.

           Kituo cha sheria na haki za binadamu nchini tanzania (LHRC) leo kimeitaka serikali kuwawajibisha viongozi ambao wamekuwa wakitoa kauli ambazo wamedai kuwa zinaonyesha dharau na kebehi kwa watanzania kwani kufanya hivyo kutaonyesha uwajibikaji kwa viongozi wa Tanzania.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dare s salaam kwa niaba ya  mkurugenzi mtendaji wa kituo cha sheria na haki za binadamu nchini Tanzania,Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia amesema kuwa kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya viongozi wa serikali kwa wananchi wao zimekuwa zikionyesha dharau na kebehi kwa watanzania na ni hali inayoonyesha kumomonyoka kwa maadili miongoni mwa viongozi wa Tanzania.

Amesema kuwa kumekuwa na kauli za dharau na kejeli ambazo zimekuwa zikitolewa kwa wananchi kutoka kwa viongozi wao pale ambapo wananchi  wanapohoji mambo ya msingi na kumekuwa hakuna hatua zozote ambazo zimekuwa zikichukuliwa kwa viongozi hao jambo ambalo amesema kuwa linawapa kiburi kuwa hakuna yoyote anayeweza kuhoji.
 Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.

Akitolewa mfano wa baadhi ya kauli ambazo zimewahi kutolewa na viongozi wa Tanzania amesema kuwa moja ya kauli ya kuudhi iliyotolewa katika sakata la pesa za ESCROW ambayo ilitolewa na aliyekuwa waziri wa ardhi ANNA TIBAIJUKA ambapo wakati akihojiwa na baraza  la maadili alisema kuwa “HIYO MILLION KUMI SI NI PESA YA MBOGA TU”kauli ambayo amesema kuwa inaudhi ukizingatia kuwa watanzania wengi wanaishi chini ya dola moja.

Kauli nyingine zilizotolewa na viongozi mbalimbali wakati wakijitetea katika ukwapuaji wa fedha za ESCROW ni pamoja na “SIKUMWOMBA JAMES RUGEMALILA ANIWEKEE HELA,NA SIJUI KWA NINI ALINIWEKEA HELA HIZO,HATA ALIVYONIAMBIA NIFUNGUE ACCOUNT BANK YA MKOMBOZI ILI ANIWEKEE FEDHA HIZO SIKUMUULIZA FEDHA HIZO NI ZA NINI”
Kauli nyingine ni ile inayosema “NINA ACCOUNT NYINGI NA ZA NJE YA NCHI NINGETAKA NINGEMWAMBIA AZIWEKE FEDHA ACOUNT ZA HUKO”.

Amesema kuwa kauli hizo zilizotolewa katika sakata la kuwahoji wahusika wa ukwapuaji wa fedha za ESCROW ni mwendelezo wa kauli ambazo zimewahi kutolewa na viongozi kipindi cha nyuma kama kauli aliyowahi kuitoa waziri CHENGE KUWA “hivi ni vijisent tu”na ile ambayo aliitoa waziri MAGUFULI ya kuwataka wananchi wa kigamboni kama watashindwa kulipa mia mbili ya kuvuka na panton bora waogelee kauli ambayo iliwaacha baadhi ya watanzania midomo wazi kwa kusikia kauli kama hivyo kwa kiongozi waliyemchagua.

Amesema kuwa kwa kauli hizo ni wazi kuwa Tanzania bado ina tatizo kubwa katika katika swala la uongozi na uwajibikaji wa viongozi katika mfumo mzima wanchi.

Aidha amesema kuwa ili kukabiliana na changamoto hii ya viongozi wa Tanzania ni lazima sheria ya maadili ya viongozi wa umma itekelezwe kama ilivyoanishwa na secretarieti ya maadili ya viongozi wa umma,ikiwa ni pamoja na viongozi kuwajibishwa kwa kauli zao zenye kuonyesha dharau kwa wananchi wa Tanzania.

Katika hatua nyingine bwana sungusia amesema kuwa ikiwa Tanzania inaelekea katika mchakato wa kupata katiba mpya lakini bado katiba iliyopendekezwa kwa ajili ya kupigiwa kura haijashinikiza uwepo wa uwajibikaji kwa viongozi watakaochaguliwa kwa ajili ya kuwatumikia watanzania hivyo bado katiba ijayo haiwezi kuwa dawa ya tatizo hilo nchini.

Miaka ya hivi karibuni kumeibuka kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na viongozi wa tanzania ambazo zimekuwa zikionekana kama ni dharau kwa watanzania jambo ambalo limeanza kupigiwa kelele na wanaharakati wengi wakidai kuwajibishwa kwa wanaotoa kauli hizo.

Post a Comment

Previous Post Next Post