Mwenyekiti
wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, ameiomba
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, kutoa amri kwa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kusitisha kujadili suala lolote
linalohusu kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi.
Mtikila
aliwasilisha maombi yake jana mbele ya jopo la majaji watatu
likiongozwa na Mwenyekiti, Jaji Richard Mziray, anayesaidiana na Jaji
Lawrence Kaduri na Said Kihio.
Kesi ya msingi ambayo Mtikila anaomba Mahakama ya Kadhi isiruhusiwe nchini, ilipangwa kutajwa jana.
Upande
wa Jamhuri uliongozwa na Mawakili wa Serikali Wakuu, Gabriel Malata na
Kasori Sarakikya, ulidai kuwa utawasilisha majibu ya maombi ya Mtikila
leo.
Mtikila
alidai kuwa anaomba kuwasilisha hati ya dharura mahakamani akitaka
bunge hilo lisijadili wala kuzungumzia suala la Mahakama ya Kadhi.
“Ina maana suala hili baada ya kufunguliwa mahakamani linajadiliwa huko nje ya Mahakama?,” alihoji Jaji Mziray na kuitikiwa na Mtikila.
Jopo
hilo lilisema upande wa Jamhuri uwasilishe majibu ya maombi ya Mtikila
kwa njia ya maandishi leo na kesho kesi hiyo itatajwa.
Mtikila
alifungua kesi ya madai kupinga kitendo cha serikali kupeleka muswada
bungeni wa kutunga sheria ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi, kwamba
kuanzishwa kwake ni kinyume cha Katiba ya nchi.
Mtikila
ameiomba Mahakama itoe amri kwamba wale walio kwenye mamlaka ya
serikali akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais (Mahusiano na Uratibu), Mary Nagu; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk.
Asha-Rose Migiro; Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na Waziri
wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira na wenzao, watoe sababu
kwa nini wasifungwe kifungo kisichopungua miaka mitano ikiwa watashindwa
kujieleza.
Pia,
Mtikila kupitia hati yake ya madai iliyopewa usajili namba 14 ya mwaka
huu, ameomba Mahakama itoe amri ya vigogo hao kufungwa kifungo hicho
kutokana na kuchezea Katiba ambayo ni sheria mama ya nchi.
Katika
hati yake, Mtikila pia anaiomba Mahakama itoe amri kwamba Mahakama ya
Kadhi na Jumuia ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC), itangaze kuwa ni haramu
kwenye ardhi ya Tanzania.
Pamoja
na mambo mengine, Mtikila anadai kuwa suala la serikali kuandaa Muswada
wa Kiislamu na kuuwasilisha bungeni na kitendo cha Bunge kukubali zaidi
ya kuukataa ni sawa na uhaini, kinachofanywa na waliopanga kuupeleka
muswada huo bungeni.
Anaendelea
kudai kuwa kitendo hicho ni sawa na uvunjifu mkubwa wa viapo vya
viongozi hao walivyoapa wakati wa kushika nafasi za uongozi wa umma na
ni kinyume cha kifungu cha 19 cha Katiba ya nchi kinachoeleza kwamba
masuala ya dini na kuabudu yatakuwa ni ya mtu binafsi na kuongeza kuwa
uendeshaji wa mambo au taasisi za kidini hazitakuwa sehemu ya mamlaka ya
nchi
Post a Comment