Katibu
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amesema wizi
ndani ya Serikali ni moja ya mambo mawili yanayoangusha chama hicho na
amewataka wanachama wake kutokaa kimya na badala yake, kupigia kelele
vitendo vya wizi kwa watendaji wa Serikali.
Katika
hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo ameeleza kukerwa na dhana ya utawala
bora, ambayo amesema imekuwa ikitumiwa kama kivuli cha kulinda wezi wa
mali ya umma, kwa maelezo kuwa ni ngumu kuwafukuza madarakani au
kuwaadabisha bila kufuata sheria.
Alisema
hayo alipozungumza na wanaCCM wa Jimbo la Kibakwe mkoani Mpwapwa, akiwa
katika ziara ya kutembelea Mkoa wa Dodoma kukagua shughuli mbalimbali
za maendeleo, ikiwemo utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2010.
"Yapo
mambo yamewaudhi Watanzania wengi. Kwanza ni suala la wizi serikalini.
Eti mtu kaiba halafu sisi tunaanza kupiga maneno mara ooh kaiba au
hajaiba? Aondoke asiondoke?
“Tumwadhibu
tusimwadhibu? Ukweli ni kwamba mtu akituhumiwa, tuhuma peke yake
inatosha kumfanya aondoke na kama hataki basi tumuondoe kwa nguvu na si
kuleta maneno,” alisema na kuongeza kuwa enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, dhana hiyo haikupewa nafasi kwa wezi.
"Lazima
niseme wazi, Watanzania wametushangaa sana katika hili, mwingine akiiba
kuku si sawa… wakubwa serikalini wanasema afungwe, lakini huyu aliyeiba
fedha nyingi za umma tunasema utawala bora!
“Lazima
tulikatae hili kwa nguvu zote na mtu wa kwanza anayepaswa kukasirika ni
mwanaCCM, kuweni wakali acheni kabisa kulindana," alisema Kinana.
Akionesha
wazi kukerwa na hali hiyo, Kinana alisema kinachosikitisha zaidi ni
kuona mtendaji ndani ya Serikali anapoiba, wanajitokeza wanaCCM wengine
ili kumkingia kifua asichukuliwe hatua, jambo ambalo limekuwa likiwakera
Watanzania wengi.
"Mtu
ameiba wazi kabisa, wanatokea wanaCCM wenzake utasikia oooh hakujua,
ooh tumuonee huruma. Jamani huyu mtu hakujua kwani hana macho kuona
anachokifanya ni wizi?
“Nawaomba
wanaCCM simamieni uadilifu, mmechaguliwa na wananchi kutokana na imani
yao kwenu na kama tunavyofahamu imani huzaa imani, nataka niahidi CCM
tutakuwa wakali sana ukiiba lazima uondoke," alisema Kinana.
Akielezea
kukerwa na matumizi ya dhana ya utawala bora, Kinana alisema dhana hiyo
katika siku za hivi karibuni imeanza kutumiwa, ili kulinda wezi wa mali
ya umma wasichukuliwe hatua na kuadhibiwa kwa makosa wanayoyafanya.
"Siku
hizi kuna hiki kitu kimezuka kinaitwa utawala bora. Wakati mtu anaiba
hafuati utawala bora, lakini akishaiba na kukamatwa utasikia lazima
tufuate utawala bora, mara tuunde Tume, mara mpeni muda wa kujitetea,
huyu mtu keshaiba unapompa nafasi na tena kama ana fedha alizoiba
anaweka mawakili hata wanne.
"Huu
utawala bora ni lazima sasa tuutazame kwa macho mawili maana ni kama
umeegemea upande mmoja. Mtu anaiba kuku hakuna utawala bora, lakini
anaiba mali ya umma, unaambiwa kuna utawala bora! Mwizi dawa yake ni
jela si maneno, lazima tujenge utamaduni wa kuwajibishana.
"Lazima
tuige wakati wa utawala wa Baba wa Taifa, yeye alisema ukikosea iwe ni
sawa na kugusa moto, ukigusa moto adhabu ni palepale, ilikuwa ukibainika
tu unastaafishwa kwa manufaa ya umma, lakini sasa unaambiwa utawala
bora.
"Mtu akiiba anahamishwa… chama chenye misingi imara siku zote kitaheshimika, kitaaminiwa na kitakaa madarakani kwa muda mrefu.
"Mkilindana
wanaCCM na Iyena Iyena zenu hamtafika mbali, ni lazima sasa tuwe
wakali. Wengi wa wanaCCM ni masikini, na wachache kama 100 au 20 hivi
ndio matajiri. Wanaiba, matajiri wachache wanaoishi maisha ya mbinguni,
adhabu wanapata masikini wengi wanaoishi duniani, hili halikubaliki.
"WanaCCM
jumla yetu tupo milioni saba lakini hawa wezi wapo kama 100 au 20,
tusiyumbishwe na watu hawa wachache, mimi ni Katibu Mkuu wa Chama cha
wakulima masikini na wafanyakazi masikini sitakubali kuona chama changu
kinageuzwa dampo la walanguzi," alisema Katibu Mkuu huyo wa CCM.
Kwa
upande mwingine aliwataka wanaCCM kutembea kifua mbele kutokana na
utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ya mwaka 2010, kutokana na mambo mengi
yaliyoahidiwa katika Ilani hiyo kutekelezwa japo alikiri kuwepo kwa
changamoto kadhaa.
"Kama
kuna kasoro waite wananchi waambie, kama tunapongezwa kwa mazuri
tuliyoyafanya ni lazima tukubali kuulizwa maswali kwa yale ambayo
hatujayatekeleza. Sio unataka upongezwe kwa mazuri tu lakini mabaya
tunayakwepa," alisema Kinana.
إرسال تعليق