Wakati joto la mbio za kuwania urais likiendelea kuisisimua
nchi, Umoja wa Wanawake Wanasiasa Tanzania (Ulingo), kwa kushirikiana na
Mtandao wa Wanawake na Katiba, umesema tayari wameandaa majina matano
ya wanawake kuwania nafasi hiyo baadaye mwaka huu.
Mwenyekiti wa Ulingo, Anna Abdallah bila kutaja
majina ya wagombea hao wanawake, alisema jana kuwa waliopendekezwa,
baadhi wanatoka nje ya vyama vya siasa.
Hata hivyo, ingawa hakutaja majina ya wateule hao,
wadadisi wa mambo ya siasa wanalitaja jina la Waziri wa Katiba na
Sheria, Dk Asha-Rose Migiro kuwa miongoni.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), Dk Hellen Bisimba alisema wameanzaa kampeni hizo tangu Septemba
mwaka jana kupitia mradi wa ‘Wanawake na Uchaguzi’.
“Tumeshazunguka mikoa 15 nchini kutoa elimu kwa
wananchi kuunga mkono harakati za wanawake katika Uchaguzi Mkuu,”
alisema Bisimba.
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Lihundi
alisema ataunga mkono jitihada za wanawake kuwania nafasi za uongozi na
atafanya hivyo bila kujali itikadi za vyama.
Hadi sasa tayari wanasiasa kadhaa wameonyesha nia
ya kuwania nafasi hiyo ya ukuu wa nchi. Miongoni mwao ni Bernard Membe,
Edward Lowassa, Khamis Kigwangalla, Januari Makamba, Samuel Sitta,
Frederick Sumaye, Stephen Wasira na Mwigulu Nchemba wote kutoka CCM.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu
Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Penina Mlama
alisema Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza kuingia kwenye mabadiliko ya
kuongozwa na mwanamke. “Kuna nchi kama Liberia na Brazil, hizi
zinaongozwa na marais wanawake na wanafanya vizuri. Sisi pia tuna
wanawake wenye uwezo wa kuongoza, sioni shaka yoyote.”
إرسال تعليق