Zaidi ya wakazi 1,163 wa eneo la Buguruni kwa Mnyamani hawana mahali pa kuishi baada ya nyumba zao 517 kukumbwa na mafuriko.
Akizungumza jana na gazeti hili, Mwenyekiti wa
Mtaa wa Buguruni kwa Mnyamani, Abdallah Mng’ae alisema maji hayo
yanaendelea kuongezeka na madhara zaidi yanaweza kutokea kutokana na
mvua kuendelea kunyesha.
Alisema siku ya kwanza, nyumba 30 zilikumbwa na mafuriko, lakini kadri mvua inavyozidi kuendelea ndivyo maafa nayo yanaongezeka.
“Wengi wao waliokumbwa na mafuriko hayo kwa sasa
wanalala katika vibaraza vya watu wakiwa na watoto wadogo, wanapigwa na
baridi usiku kucha,” alisema Mng’ae na kuongeza:
“Hadi sasa hawajapata msaada wowote kutoka serikalini, tunaomba msaada hasa chakula, mavazi na dawa.”
Alisema watu waliojitokeza kutoa msaada ni
Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba
aliyetoa Sh500,000.
Eneo la Vingunguti, mwandishi alishuhudia nyumba
nyingi zikiwa zimejaa maji, huku wamiliki wakilalamika kuwa vitu vingi
vimeharibika.
Mkazi wa eneo hilo, Amina Salehe alisema tangu
juzi hadi jana maji ya mvua yameendelea kuingia ndani ya nyumba yake na
kumsababishia kukosa sehemu ya kulala.
Wakati huohuo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
(TMA), imesema mvua itaendelea kunyesha kwa siku tatu mfululizo katika
mikoa ya Pwani, Mtwara, Lindi, Dar es Salaam na Tanga.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Hali
Hewa jana, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agness Kijazi aliwataka wananchi
wanaoishi mabondeni kuhama ili kuepuka madhara yanayoweza kuwakumba.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Samwel Mwampashe alisema polisi wanaendelea kufanya doria ili kubaini madhara zaidi.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni,
Camillius Wambura alisema hawajapata taarifa ya kutokea kwa vifo mkoani
humo zaidi ya zile za baadhi ya watu kukosa makazi baada ya nyumba zao
kujaa maji.
إرسال تعليق