Mnenguaji mahiri na mkongwe nchini, Lilian Internet(35), amesema
vijana wengi walio katika fani hiyo wanajihusisha na matumizi ya dawa
za kulevya.
Nyota huyo, mzaliwa wa Mkoa Kilimanjaro, pia
amelaani tabia ya baadhi ya vijana kuwa na wapenzi wengi huku akisema
anamshukuru Mungu kwa kuwa ameweza kujiepusha na tabia hiyo na sasa ni
mke wa mtu.
“Asilimia kubwa ya wanenguaji wanatumia dawa za
kulevya, si kwa sababu wanatumia dawa hizo ili wacheze vizuri jukwaaani,
bali waliingia huko kwa kufuata mkumbo. Jambo hilo silifurahii
linaniumiza sana,” anasema Internet.
Mnenguaji huyo ambaye jina lake halisi ni Lilian
Josephat Tungaraza anasema tatizo hilo ni kubwa na vijana wengi, hasa
wasichana wameangukia katika tabia hiyo kwa kudanganywa na wanaume na
wakati mwingine wao wenyewe kuwa watapata nguvu zaidi za kucheza
jukwaani.
“Mimi nafanya vizuri na mashabiki wengi
wanafurahia kazi yangu tangu nilipojiunga na Bendi ya Twanga Pepeta
mwaka 1997 ilipoanza. Mpaka leo wengi wakiniona wanadhani nina miaka 20,
lakini hii yote inatokana na kujali afya yangu. Naomba Mungu awajalie
ili watokane kwenye matumizi ya dawa za kulevya kwani wengi
wanadhalilika, hiyo inaniumiza,” anasema.
Lilian anasema mama yake ambaye ni mwenyeji wa
Mwanga mkoani Kilimanjaro, amekuwa na mchango mkubwa katika maisha yake
kutokana na kumuunga mkono kwa kazi anayoifanya, hivyo kusaidia kuwa
naye karibu katika mambo mbalimbali.
“Wakati wa kwenda kazini, kuna vyakula
ninavyotakiwa kula ambavyo sivitumii sana. Sina ulevi ninaotumia zaidi
ya bia mbili kwa siku. Vilevi vilivyokatazwa mimi situmii,” anasema.
Msanii huyo anaeleza kuwa hunywa baada ya kazi au wakati mwingine akiwa nyumbani siku ya Jumatatu ambayo ni mapumziko kwake.
Akizungumzia mafanikio yake anasema: “Ni kujitunza
kwa sababu hii ni kazi ngumu. Kuna vitu unatakiwa kuwa unavifahamu na
kutekeleza; kwanza ni kulala mapema, kuwa na kiasi katika utumiaji wa
pombe, lakini pia kutokuwa na wanaume wengi kwani hiyo inakufanya pia
upoteze mwelekeo.”
Kauli hiyo inaungwa mkono na Mkurugenzi wa Twanga
Pepeta International Asha Baraka anayesema: “Tumeona wasanii wengi wa
Tanzania ambao awali walikuwa wanafanya vizuri, lakini baada ya kujaa
sifa na kukutana na marafiki wengi hasa makundi, wakazama kwenye dawa za
kulevya, sasa wanatapatapa na kubaki kulaumu, wakati wenyewe
wamejiharibia.”
Hata hivyo, Asha anasema Twanga Pepeta imekuwa
ikitoa mafunzo kwa wasanii ili kujiweka kando na matumizi ya dawa za
kulevya kupitia vikao vyao wakiwataka pia kuwa na nidhamu ya kazi.
“Nidhamu ya kazi ni jambo linaloingia katika haya
yote. Nimekuwa nikiwaashauri wasanii wangu katika haya na mara nyingi
tumefanya hivyo ndiyo maana unaona Twanga Pepeta imesimama mpaka leo,
mengine yanatokana na msanii mwenyewe kujibana katika makundi
yasiyofaa,” anasema Asha Baraka.
إرسال تعليق