Waziri Mkuu wa zamani, Fedrick Sumaye.
Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani,
imewataja vigogo wanaohodhi maeneo makubwa ya ardhi bila ya kuyaendeleza
na kuwapa siku 90 kuhakikisha wanayaendeleza, kinyume chake
yatachukuliwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Tatu
Suleiman, ilisema vigogo hao walinunua mashamba katika eneo hilo na
kisha kuyaacha kwa muda mrefu bila kuyaendeleza akiwamo mke wa Waziri
Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Mama Ester Sumaye ambaye
anamiliki mashamba mawili, moja likiwa na ukubwa ekari 145.5 likiwa na
namba 6069 na 6070 na shamba la pili lenye ukubwa wa ekari 103. 25
likiwa na namba 6071 na 6075, yote yakiwa Misufini, Kibaha vijijini.
Taarifa hiyo inawataja watu wengine maarufu ambao wameshindwa
kuyaendeleza mashamba hayo kuwa ni, Phillipo Marmo ambaye ni Balozi
wa Tanzania nchini Ujerumani anayemiliki shamba 6159-6164 maeneo ya
Kikongo, Nicodemus Banduka ambaye ni mkuu wa mkoa mstaafu wa mikoa ya
Pwani, Iringa na Mtwara anaye miliki shamba namba 1707 eneo la Vikuge
ambalo alilipata mwaka 2,000 na Kipi Warioba aliyewahi kuteuliwa
kugombea Ubunge Jimbo la Kawe ambaye anamiliki eneo Mperamumbi lenye
ukubwa wa heka 4000.
Taarifa hiyo inaonyesha kuwa, watu wengi walichukua mashamba katika
eneo hilo kuanzia miaka ya 1986 na kushindwa kuyaendeleza
na kusababisha kuwa mapori hali iliyopelekea halmashauri hiyo kufuata
sheria na kanuni zinazohusiana na umiliki wa ardhi.
Kufuatia mashamba hayo kutelekezwa, halmashuri ya wilaya hiyo
inapanga kuwasilisha taarifa hiyo kwa wizara husika ili miliki zake
zifutwe endapo wahusika watashindwa kuyaendeleza kwa muda
waliopewa.
Tatu, alisema mwaka jana waliwataka watu wote waliochukua mashamba
hayo kuyaendeleza baada ya kufanyiwa uhakiki na baadhi ya
watu walijitokeza kuyaendeleza, lakini watu zaidi ya 40 hawajitokeza.
“Kutokana na kukahidi kuyaendeleza mashamba hayo, tumeshapeleka
majina ya wamiliki Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
na wizara imetutaka tutoe tena siku 90 kama hawatatekeleza kwa kipindi
hicho, watajua nini cha kufanya,’’ alisema.
Gazeti hili lilipowasiliana na Waziri Mkuu wa zamani, Sumaye kwa
njia ya simu ili kuzungumzia taarifa za mkewe kushindwa
kuyaendeleza mashamba hayo kwa kipindi kirefu, alisema hana taarifa
zozote za mkewe kushindwa kuyaendeleza mashamba hayo anayomiliki.
‘‘Wewe ndiyo nakusikia, sisi hatujaliona hilo tangazo, wala mke
wangu hana hizo taarifa ila baadaye tutakapoziona tutakupigia simu
tuwasiliane,’’ alisema Sumaye.

Wamo Balozi Philip Marmo, Nicodemus Banduka.
إرسال تعليق