Hivi karibuni, Taasisi ya Repoa ilitoa utafiti wake unaoonyesha
kuwa hali ya kiuchumi ya wananchi inazidi kuwa mbaya ikilinganishwa na
ilivyokuwa miaka 10 iliyopita.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa, licha ya pato la taifa
kuendelea kuongezeka hadi kufikia asilimia saba, Watanzania wengi
wanaamini kwamba hali ya uchumi nchini mbaya.
Utafiti huo wa Afrobarometer, awamu ya sita
uliofanywa kati ya Agosti 26 na Septemba 29 mwaka jana, walihojiwa
Watanzania 2,386 wa Tanzania Bara na Visiwani. Wananchi hao walisema
kuwa hali ya maisha inazidi kuwa mbaya ikilinganishwa na ilivyokuwa
mwaka 2003.
Akitoa ripoti ya utafiti huo, Dk Lucas Katera
kutoka Repoa, anasema wananchi wanalalamika kuwa licha ya Serikali
kusema kuwa uchumi ni mzuri na kwamba nchi inapiga hatua ikilinganishwa
na ilivyokuwa, wanaona watu wachache tu ndiyo wanaonufaika na maendeleo
hayo.
Akitoa mfano anasema mwaka 2003 asilimia 42
walisema hali ya uchumi ilikuwa mbaya, mwaka 2005 asilimia 38, utafiti
uliofuata mwaka 2008 idadi ya wananchi iliongezeka na kufikia asilimia
57 huku mwaka jana walikuwa asilimia 67.
“Idadi ya wananchi wasioridhishwa na namna
Serikali inavyotekeleza miradi ya huduma za kijamii imeongezeka.
Wananchi wanne kati ya kumi hawafurahishwi na huduma ya maji
inayotolewa,” anasema Dk Katera.
Mtafiti huyo anasema matokeo hayo yamebaini kuwa
kuna uhusiano wa karibu kati ya hali mbaya ya kiuchumi na utoaji mbaya
wa huduma za jamii.
“Wananchi saba kati ya kumi wanasema Serikali
inafanya vibaya kwenye sekta ya maji na elimu jambo linalosababisha hali
mbaya ya kichumi,” anasema.
Mtaalamu wa Sera na Bajeti, Gilead Teri anasema
wananchi wanahoji juu ya sababu zinazofanya matumizi ya Serikali
kutowekwa wazi. Wanapendekeza uwazi zaidi uongezwe kwenye masuala
yanayohusu umma.
“Wengi wamekata tamaa, wanasema takwimu hizo
haziendani na hali halisi ya kipato chao. Hapa Serikali inapaswa
kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za jamii,” anasema.
Teri anasema kukithiri kwa rushwa ni moja ya changamoto zinazowafanya wananchi kutokuwa na imani na Serikali.
Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe,
Dk Prosper Ngowi anasema uchumi unaweza kukua, lakini kama hakutakuwa na
matumizi sahihi ya fedha za umma wananchi wataendelea kuona kasoro za
kiuchumi.

إرسال تعليق