Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MBUNGE
wa Viti Maalum (CCM), Al Shaimaa Kweigyir, ameitaka serikali
kuhakikisha kwamba hukumu za watu wanaokutwa na hatia dhidi ya watu
wenye ulemavu wa ngozi (albino), zinafanyika kwa uwazi, sambamba na
kutocheleweshwa ili kulinda roho za Watanzania wanaoendelea kuangamia.
Al-Shaimaa
aliyasema hayo bungeni jana wakati akitoa maelezo binafsi kwa kupitia
Kanuni ya Kudumu ya Bunge ya (50) 1 inayomtaka mbunge kwa ruhusa ya
Spika kutoa maelezo binafsi yanayomhusu au yanayoigusa jamii moja kwa
moja.
Mbunge
huyo ambaye pia ni mlemavu wa ngozi alisema kwamba endapo hukumu za
kesi za wahalifu wa albino zitahukumiwa mapema na kwa uwazi itatoa funzo
kwa wengine wanaofikiria kufanya unyama dhidi ya albino hapa nchini.
Mbunge wa Viti Maalumu, Al-Shaymaa Kweigyir, akiomba mwongozo wa Spika bungeni jana mjini Dodoma, kutaka hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya watuhumiwa wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).
Akiendelea kuongea kwa msisitizo juu ya mauaji ya albino Tanzania.
“Na
mimi ni mhanga katika jambo hili kwa sababu watu wanaishi kwa mashaka,
hivyo naomba hukumu za wahalifu hao ziwe wazi kila mtu aone ili iwe
fundisho kwa waliofanya na wale wanaofikiria siku moja wajiingize kwenye
unyama huo.
“Pia
naomba sheria za mauaji zirekebishwe ili kulinda haki za walemavu mara
baada ya kufanyiwa unyama sambamba na kuwapa adhabu kali wale wote
wanaokutwa na hatia dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi,” alisema
Kweigyir.
Kweigyir
ni miongoni mwa wabunge wanaopigania haki za kuishi za watu wenye
ulemavu wa ngozi, likiwa ni janga lililoshika kasi katika maeneo kadhaa
ya Tanzania, hususan katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kunakoonekana
kushamiri vitendo vya kuwadhuru na kuwaua walemavu hao wa ngozi.
Post a Comment