MBUNGE
wa Korogwe Vijijini, Bw. Stephen Ngonyani (CCM) ambaye pia ni Mjumbe wa
Baraza la Umoja wa Wazazi Taifa, amesema wakati huu wa kuelekea
Uchaguzi Mkuu, hapaswi kutafutiwa marafiki wala ndugu walioonesha
dhamira ya kuwania uongozi ndani ya chama na kuwaunga mkono.
Alisema
kitendo chake cha kwenda nyumbani kwa mwanachama wa CCM anayedaiwa
kutaka kuwania nafasi ya urais kwenye Uchaguzi Mkuu, kisitafsiriwe
vibaya au kuchafuliwa kisiasa.
Bw.
Ngonyani aliyasema hayo mjini Dodoma jana siku moja baada ya Jumuiya ya
Wazazi Taifa, kutoa mwezi mmoja kwa baadhi ya wajumbe wa Baraza la
Wazazi akiwemo mbunge huyo kuomba radhi kwa kutumia jina la jumuiya hiyo
vibaya.
Jumuiya
hiyo inadai baadhi ya wajumbe hao ni miongoni mwa makundi ya watu
waliokwenda nyumbani kwa mwanachama wa CCM, kumshawishi achukue fomu ya
kuwania urais na kumchangia fedha wakitumia jina la jumuiya.
Tamko
la jumuiya hiyo lilitolewa na Mwenyekiti wake, Bw. Abdallah Bulembo,
akimtaja Bw. Ngonyani kuwa miongoni mwa wajumbe wa baraza wanaopaswa
kuomba radhi bila kumtaja mwanasiasa aliyetembelewa akisema ni mtu
anayefahamika na wengi.
Akijibu
tuhuma hizo, Bw. Ngonyani alisema yupo tayari kwa lolote; lakini hawezi
kuomba radhi kwani yeye pamoja na wenzake walikwenda nyumbani kwa
Mbunge huyo wa Monduli, mkoani Arusha, Bw. Edward Lowassa; si kwa
kutumia nembo ya jumuiya hiyo.
"Hatukwenda
nyumbani kwa Lowassa kuomba fedha au chakula; bali tulikwenda kwa
mapenzi mema...mimi kama ilivyo kwa wajumbe wengine, nilipata taarifa za
kwenda kumsalimia Bw. Lowassa nyumbani kwake.
"Kwa
sababu ya ukaribu wangu na Lowassa, sikusita kwenda lakini si kwa
kuwakilisha nembo ya jumuiya hiyo na wala hatukuhongwa kufanya hivyo," alisema Bw. Ngonyani.
Alisema
yeye kama mbunge, atamshabikia mtu ambaye yupo ndani ya roho yake na
kuongeza kuwa, ataendelea kwenda kwa Bw. Lowassa hadi kieleweke na kama
kuna
hatua za kuchukuliwa dhidi yake yupo tayari na huyo anayesema wao wana makosa naye ajichunguze.
"Nashangaa
kusikia mimi ndiye niliyetoa fedha na kuwapa wajumbe wenzangu
tuliokwenda nyumbani kwa Lowassa jambo ambalo linanisikitisha sana kwa
mtu maskini kama mimi kutafuta watu niwape fedha ili waende kwa Lowassa.
"Tulienda
kwa mapenzi yetu kupitia umoja ambao tulikuwa tumekubaliana, nipo
tayari kukosa ubunge, naweza kurudi katika fani yangu ya uganga, kabla
sijawa mbunge nilikuwa huko; lakini viongozi mbalimbali walinishawishi
nigombee ubunge na kuipata nafasi hiyo," alisema.
Mjumbe
mwingine wa baraza hilo mkoani Njombe, Evarist Lupenda, alisema yeye ni
miongoni mwa watu waliokwenda nyumbani kwa Lowassa kwa matakwa yake si
kushawishiwa.
Alisema
yeye na wenzake walipewa taarifa ya kwenda kwa Lowassa kumsalimia na
hawakutumia jina la jumuiya hiyo na matamko yaliyotolewa hayakuwa ya
jumuiya.
Aliongeza
kuwa, kama imefikia hatua ya kutishana wakati huu wa kuelekea Uchaguzi
Mkuu, viongozi wengi ambao tayari wameonesha kuwa karibu na Lowassa
akiwemo Mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, Hamis Mgeja, Mgana Msindai
wa Singida, basi chama kiwachukulie hatua na hao.
"Bulembo lazima azifanyie uchunguzi taarifa anazopelekewa kabla ya kutoa matamko," alisema.
Naye
mjumbe wa baraza hilo mkoani Dodoma, Mchungaji Damas Mkasa, alisema sh.
600,000 walizomkabidhi Bw. Lowassa ili kumshawishi achukue fomu
walijichangisha wenyewe sh. 20,000 kila mmoja na hazikutolewa na Bw.
Ngonyani.

Post a Comment