Maaskofu
na wachungaji wa makanisa ya kipentekosti wakiingia ukumbini katika
Hoteli ya Tamari iliyopo Mwenge tayari kwa kutoa tamko lao.
Katibu
wa Maaskofu wa makanisa ya Kipentekosti Dk. Damas Mukassa akisoma tamko
la maaskofu hao Dar es Salaam jana, kuhusu sakata la kukamatwa kwa
Askofu wa Kanisa la Uzima na Ufufuo, Josephat Gwajima ambalo leo hii
wanatarajia kwenda kumuona Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Mangu
kuzungumzia suala hilo. Kulia ni Askofu Dk.Mgullu Kilimba na Askofu
Mwaviga Mwafululila.
Askofu Dk. Paul Shemsanga akizungumza katika mkutano huo ambapo maaskofu hao walitoa tamko lao.
Wachungaji mbalimbali wakiwa kwenye mkutano huo.
Wachungaji mbalimbali wakiwa kwenye mkutano huo.
Wanahabari wakisubiri kuchukua taarifa hiyo.
Baadhi ya maaskofu wakiwa kwenye mkutano huo.
Mpiga picha wa gazeti la Mtanzania, Hamphrey Shao akipiga picha katika mkutano huo.
Na Dotto Mwaibale MAASKOFU
wa makanisa mbalimbali ya Kipentekoste nchini wamesema wanatarajia
kwenda kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Ernest Mangu ili
kulimaliza sakata la Askofu Josephat Gwajima, kwani kuliendeleza ni
kuleta mpasuko wa kidini katika jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,
Katibu wa Maaskofu hao, Askofu Dk. Damas Mukassa alisema hakuna sababu
ya jambo hilo kukuzwa, kwani mhusika amemsamehe Askofu Gwajima.
Dk. Mukassa alisema ni vema Serikali na vyombo vya usalama
vikatumia weledi katika kushughulikia mambo ya kidini na viongozi, kwani
yanaweza kusababisha chuki baina yao.
“Tunaomba Serikali isaidie kuondoa mkanganyiko huu, na busara
itumike ili kuepusha uvunjifu wa amani katika jamii,” alisema Mukassa.
Katibu huyo alisema wanasikitishwa kukamatwa kwa wasaidizi wa
Gwajima, kwa kisinginzio kuwa, walitaka kumtorosha, jambo ambalo
haliwezekani.
Alisema wamekaa na kutafakari kilichomkuta Askofu Gwajima,
kwani kiuhalisia afya yake ilikuwa salama, hivyo wamebaki na shaka, kama
vyombo vya usalama si sehemu salama kama zamani.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima,
Gwajima aliyelazwa katika Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam
amejitokeza hadharani na kusema kuwa, hakuna njama ya yeye kutoroshwa
na wachungaji wake na amekiri kuwa, bastola iliyokutwa katika begi ni
yake na anaimiliki kihalali.
Alisema iwapo angekuwa na lengo la kutoroka nchini
angeondokea Arusha, ambapo alikuwepo, lakini aliamua kuitikia mwito wa
jeshi la Polisi na kurejea Dar es Salaam.
Askofu Gwajima alisema baada ya wachungaji wake kupata
taarifa ya kuwa, amefariki ndipo walikwenda kumwona na kumpelekea
silaha hiyo ili aweze kujilinda.
“Kwa kuwa, palikuwa na mpango huo nikawaambia wachungaji
wangu waende nyumbani kwangu na kuchukua begi lililokuwa chumbani,
ambapo ndani yake palikuwa na baadhi ya nguo na bastola ninayoimiliki
kihalali, kwani humo ndani kulikuwa na nyaraka zilizokuwa zikionesha
umiliki na vitu vingine,” alisema Gwajima.
Alisema alishangaa kuona Askari wakiwavamia wachungaji wake
na kuwafikisha kituoni kwa kosa la kutaka kumtorosha, jambo ambalo si
la kweli.
Gwajima alisema walipofika hospitalini usiku, wachungaji wake
walimfikishia begi na kuliweka ndani ya chumba, lakini walitokea watu
ambao walijitambulisha kuwa, ni askari na kuomba mzigo ulioingizwa ndani
na hapakuwa na ushindani akawapa.
Kuhusu kuzimia kwake, alitoa taarifa ya kusumbuliwa na kichwa
kwa muda mrefu bila ya kusikilizwa ili apatiwe huduma, ambapo
kilichotokea ndiyo hicho walichokiona.
Gwajima alisema alikuwa akihojiwa na Kamanda wa Upelelezi wa
Kanda (ZCO), ambapo aliendelea kumhoji huku akimpa taarifa ya kuumwa
kichwa, lakini hakumsikiliza, hivyo mpaka anaanguka na kuzimia hakujua
kilichoendelea hadi alipofikishwa hospitalini.
Askofu Gwajima alisema hana mgogoro wowote na Askofu mwenzake
na anampenda, kilichotokea alikuwa katika kazi yake ya kukemea
aliyoyasema.
Kwa upande, Dk. Willibrod Slaa, mara baada ya kumtembelea
Askofu Gwajima hospitalini hapo, alisema haingilii ugomvi wa Askofu
Pengo na Gwajima, bali anachokipinga ni upotoshaji unaofanywa na jeshi
la polisi dhidi ya raia.
Dk. Slaa alisema polisi waache maneno yao ya kusema mtu
anajifanya anaumwa, kwani ni kitendo ambacho kinaonesha kuwa,
halithamini utu wa mtu.
Aidha, alisema mambo anayofanyiwa Askofu Gwajima hata yeye
aliwahi kufanyiwa akiwa Arusha, baada ya umma kupotoshwa kuwa,
alikamatwa na silaha kana kwamba yeye ni jambazi.
“Nilikamatwa na jeshi la polisi huko Arusha, ambapo kisheria
unapokuwa na silaha unaisalimisha, nilifanya hivyo na nikaambiwa
nijisajili, lakini siku iliyofuata taarifa ikatolewa kuwa, nimekamatwa
na silaha, hivyo inaonesha jinsi gani jeshi la polisi linavyofanya hila
kwa raia,” alisema.
Dk. Slaa alisema mahakama ndiyo itakayotoa ukweli wa jambo
hilo kama ilivyotokea katika kesi ya ugaidi dhidi Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema), wakati fulani.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba
alisema kinachoonekana kwa sasa ni ukiukwaji wa haki za binadamu ambao
unaendelea kufanywa kwa vyombo vya usalama.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda
alisema anatarajia kufanya mazungumzo na Askofu Gwajima kutokana na
kauli yake ili kujua nini kilimsukuma kutoa kauli hiyo.
Akizungumzia sakata hilo la kukutwa na silaha na kuendelea
kuwashikilia wachungaji na wafuasi wa Gwajima, Kamanda wa Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema silaha hiyo haimilikiwi
kihalali na Gwajima.
Kova
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema kuwa,
silaha zilizokamatwa hospitalini katika njama za kumtorosha Mchungaji
Josephat Gwajima hazimilikiwi kihalali.
Aidha, jeshi hilo lilisema kuwa, linaendelea na upelelezi wa
watu 15 waliohusika na tukio la kufanya njama za kutaka kumtorosha
Gwajima na uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kamishna wa Polisi, Suleiman
Kova alisema wanafanya uchunguzi ili kujua kwanini walikula njama na
mbinu gani walitumia.
Alisema silaha hiyo ambayo ni bastola aina ya Berreta yenye
namba CAT5802 ikiwa na risasi tatu iliyokamatwa juzi, imebainika kuwa,
inamilikiwa kinyume cha sheria na wamiliki si halali.
“Silaha zilizokamatwa hazimilikiwi kihalali na wahusika
akiwemo Gwajima, hawamiliki kihalali, hivyo kuna kesi ya kupatikana na
silaha, ambapo ni kinyume cha sheria.”
“Pale ambapo tutagundua kuwa, kuna makosa yaliyotajwa atachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema.
Alisema kuhusu ni kwanini alipata mshtuko kuhusu suala hilo litajulikana na daktari kwa kushirikiana na mahakama.
Kamishna Kova aliongeza kuwa, upelelezi utakapokamilika na
wakili wa Serikali akikubali, washtakiwa hao watafikishwa mahakamani.
Wakati huohuo, Methusela Gwajima ambaye ni Mwanafamilia
amekemea vikali kitendo cha kutukanwa kwa Mwadhama Polycarp Kardinali
Pengo na kwamba ni kinyume cha sheria.
Alisema kitendo hicho ni cha fedheha, ni kinyume cha sheria
ya nchi na kwamba, alitakiwa kumfuata na kumweleza na si kumtukana
matusi makubwa na kumsababishia aibu kubwa.
Aliongeza, Gwajima abebe msalaba wake mwenyewe kwa kwenda
kuomba msamaha, kwani aliamua kumchafua kiongozi huyo wa kiroho, na
kwamba itamsaidia kurudisha heshima ya mwanzo aliyokuwa nayo.
(Imeandaliwa na mtandao www.habari za jamii.com)
Post a Comment