Waganda wachota mamilioni Simba

SIMBA hii hatari sana aisee! Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na namna klabu hiyo inavyopoteza mamilioni ya fedha, huku wakishindwa kutekeleza ahadi zao kwa baadhi ya wachezaji iliwayowasajili katika dirisha dogo.
Moja ya ahadi zake kwa wachezaji hao wakiwamo Waganda wanne Emmanuel Okwi, Juuko Murshid, Dan Sserunkuna na nduguye, Simon Sserunkuma ni kupatiwa nyumba za kuishi, kitu ambacho hakijatekelezwa na viongozi wa klabu hiyo na kujikuta wakipoteza mamilioni ya fedha.
Mamilioni hayo yanapotezwa na Simba kwa kuwaweka hotelini nyota wake hao na kujikuta wakilipa Sh. 6 Milioni kila mwezi kwa miezi mitatu waliopo katika Hoteli ya Sapphire, iliyopo Kariakoo wameshapoteza kisi cha Sh. 18 Milioni.
Kila mchezaji kwa siku ndani ya hoteli hiyo analipiwa kiasi cha Sh. 50,000 kwa maana hiyo kwa mwezi kila mmoja huigharimu Simba Sh. 1.5 Milioni ambayo kwa wote wanne ni sawa na Sh. 6 Milioni.
Wakati ikipoteza fedha hizo ambazo ingeweza kuwapangia nyumba kubwa nzuri uswahilini na wakaishi kwa raha zao, inaelezwa kuwa Simba bado haijawamalizia fedha za usajili baadhi ya nyota wake akiwamo beki wake Hassan Kessy ambaye mpaka sasa anaidai Simba kiasi cha Sh 15. Mil.
Mwanaspoti inazo taarifa kwamba mchezaji huyo amelipwa Sh. 20 Milioni tu kati ya Sh. 35 Milion ializoahidiwa na Simba na huku akiwa hana mahali pa kuishi na kwenda kujibanda chumba kimoja na mchezaji mwenzake ambaye ni rafiki yake..
Kibaya zaidi ni kwamba mwenzake huyo bado anaishi kwa wazazi wake.
Kiongozi mmoja wa juu kutoka ndani ya Simba, alilithibitishia Mwanaspoti kuwa fedha inayotumika kwa ajili ya wachezaji hao wa kigeni kuwaweka hotelini ni nyingi, huku akisisitiza kuwa baadhi ya wachezaji hao akiwemo Dan hafurahishwi na maisha hayo kwani anapenda kuishi na familia yake.
“Hebu fikiria Kessy anaishi kwa rafiki yake, hao wengine wanaishi hotelini, viongozi wangu wanapoteza pesa nyingi pasipo kujua, hawafikirii baadaye itakuwaje, Kessy sio kijana wa kuishi kwa rafiki yake, suala la nyumba wamekuwa wakimzungusha mpaka leo.
“Hao wengine wanakaa hotelini, mara ya kwanza walikuwa Rombo View pale Shekilango baadaye waliwahamishia Sapphire, hata kama hawalipi ‘cash’ lakini hayo ndiyo madeni yanayokuja kuibuka baadaye bila sababu za msingi,” alisema kiongozi huyo huku akisema suala la nyumba za wachezaji lilikuwa likishughulikiwa na Katibu Mkuu wa klabu hiyo.
Katibu huyo aliposakwa kwa simu na Mwanaspoti hakuweza kutoa ushirikiano Katika mahojiano ya awali na Dn Sserunkuma, aliliambia Mwanaspoti kuwa anasubiri kupewa nyumba na uongozi wa klabu yake.
Alisema kwamba mara baada ya hilo kufanyika atakachofanya ni kuileta familia yake hapa nchini ili aishi nayo pamoja.
- Mwanaspoti

Post a Comment

Previous Post Next Post