SIRI imefichuka. Mbio za Edward Lowassa, kusaka urais kwa udi na uvumba, zimebarikiwa kwa asilimia 100 na Rais Jakaya Kikwete.
Lowassa amekutana na Kikwete mara kadhaa na kufunga makubaliano ya siri
yanayolenga kumsaidia yeye kuwa mgombea urais kupitia Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
“Yote yanayofanywa na Edward (Lowassa), yamebarikiwa na Kikwete. Bila
hivyo, Lowassa asingekuwa na ubavu wa kufanya anachokitenda,” ameeleza
kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya serikali.
Kikwete ndiye Mwenyekiti wa Taifa wa CCM na Rais wa Jamhuri.
Kuibuka kwa taarifa kuwa Lowassa amefunga makubaliano na Kikwete,
kumekuja katika kipindi ambacho mwanasiasa huyo aliyeapa kufia katika
vita ya kuwania madaraka, ameanza kupokea makundi ya wananchi akidai
wanamuomba kugombea urais.
Mtoa taarifa wa gazeti hili anasema, “Kikwete na Lowassa wanakutana
sana, tena kwa siri. Wamejadili mengi, ikiwamo kinyang’anyiro cha urais.
Itakuwa ajabu, bwana huyu kutokuwa mgombea kupitia CCM.”
Waziri mkuu huyo aliyejiuzulu kwa kashfa ya mkataba tata wa kufua umeme,
kati ya serikali na kampuni ya Richmond, tayari amefungulia anaowaita
“wafuasi wake,” kushawishi baadhi ya watu kwa lengo la kutafuta kila
upenyo kuhakikisha anapata nafasi ya kushika utawala Oktoba mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa watu walio karibu na mwanasiasa huyo,
makubaliano yake na Kikwete ndiyo yanayomfanya kuwa “mbogo” hadi kuikuka
taratibu za chama chake.
Uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa Oktoba mwaka huu – kuchagua rais, wabunge na madiwani.
Hata hivyo, mtoa taarifa wa MwanaHALISI Online anasema, pamoja na kuwapo
makubaliano hayo, bado Lowassa hawezi kujihakikishia nafasi ya kuwa
mgombea.
Anasema, Lowassa anakabiliwa na kibarua kigumu kutoka kwa makundi ya yaliyopachikwa jina la “wahafidhina” ndani ya chama chake.
CREDIT:MWANAHALISI ONLINE
CREDIT:MWANAHALISI ONLINE
إرسال تعليق