Stori: Joseph Ngilisho
KUMEKUCHA! Duru za kisiasa katika Jimbo la Arusha Mjini zinaeleza
kuwa kuna uwezekano mkubwa wa mbunge anayeliongoza jimbo hilo kwa tiketi
ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Godbless Jonathan Lema
kuangushwa katika uchaguzi mkuu ujao baada ya mfanyabiashara mkubwa
(bilionea) mmoja (jina kapuni) jijini hapa, kudaiwa kutenga mabilioni ya
fedha kwa ajili kuumaliza ufalme wa Lema.
Godbless Jonathan Lema
Wapiga kura mbalimbali wa jimbo hilo waliozungumza na Uwazi Mizengwe,
wamebainisha hilo. Kuna wachache ambao wamesema Lema hawezi kung’oka
lakini wengi wao wamesema atang’oka kutokana na nguvu kubwa ya ushawishi
aliyonayo mfanyabiashara huyo ambaye atagombea kwa tiketi ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
“Lema hawezi kurudi bungeni tena maana jamaa (bilionea) kajipanga
sana na ukizingatia ni mzawa wa Mtaa wa National Milling ambaye
amewekeza katika biashara mbalimbali, anakubalika katika jamii kwani
anajitoa sana, hakika atamng’oa nakuhakikishia,” alisema mkazi mmoja wa
Arusha kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini.
Mkazi mwingine wa jimbo hilo ambaye pia hakupenda jina lake liandikwe
gazetini, alisema licha ya kufanikiwa kutimiza baadhi ya ahadi zake
lakini Lema ameshindwa kutekeleza ahadi nyingi likiwemo suala la jengo
la Machinga Complex ambalo aliahidi kulifanikisha.
“Kuna mambo mengi tu ya msingi ambayo wapiga kura tumeona
hajakamilisha hususan suala la Machinga Complex, bado ni kitendawili,
sidhani kama atapenya uchaguzi ujao na ukizingatia kuna mfanyabiashara
maarufu ambaye tayari ameonesha nia ya dhati ya kutaka kumaliza kero
nyingi za Arusha Mjini,” alisema mkazi huyo.
Kuhusu madai ya kutokamilisha ahadi ya kujenga jengo la Machinga
Complex, kwa nyakati tofauti Lema amekuwa akikaririwa na vyombo vya
habari akisema ameshindwa kuikamilisha ahadi hiyo kwa kile alichodai ni
kuwekewa mizengwe na Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Akizungumza na mwandishi wetu hivi karibuni, Lema alisema hatishwi na
vitisho vya mfanyabiashara huyo ambaye anatajwa kutaka kumpoka jimbo
hilo.
“Atapoteza fedha zake bure tu kufanya kampeni, hili jimbo bado
naamini kutokana na niliyoyafanya, wananchi wataendelea kunipa dhamana
ya ubunge,” alisema Lema
إرسال تعليق