Mambo
magumu yameibuka katika suala la kujadili uanzishwaji wa Mahakama ya
Kadhi, baada ya kutokea malumbano makali na vurugu huku idadi kubwa ya
wabunge wakiitaka serikali kuuondoa Muswada wa Mahakama ya Kadhi
usiwasilishwe bungeni.
Wabunge wengi walisema kufanya hivyo kunaweza kusababisha mpasuko na kuvunjika kwa amani nchini.
Aidha,
wamesema suala la Mahakama ya Kadhi linataka kufanywa kama mtaji wa
kisiasa kwa baadhi ya viongozi wanaotaka kuwania urais katika uchaguzi
mkuu mwaka huu ili kutafuta kura za Waislamu.
Mvutano
huo uliibuka jana wakati wa semina ya wabunge kujadili Muswada wa
Sheria mbalimbali wa mwaka 2014 ambao ndani yake kuna Muswada wa
Mahakama ya Kadhi ambao umepangwa kuwasilishwa Aprili Mosi mwaka huu
siku ya kuahirisha mkutano wa 19 wa Bunge.
Mbunge
wa Ngara (CCM), Deogratias Ntukamazina, alisema Kamati ya Katiba Sheria
na Utawala ilipowaita viongozi mbalimbali wa dini kuzungumzia suala
hilo Waislamu walitofautiana katika suala la uteuzi wa Kadhi kufanywa na
Mufti Mkuu wa Tanzania na wakataka waelewane kwanza kabla ya suala hilo
kupelekwa bungeni.
Alisema
katika mkutano huo makundi 11 ambayo hayakubaliana na Baraza Kuu la
Waislamu Tanzania (Bakwata), walisema Muswada wa Mahakama ya Kadhi
uletwe bungeni baada ya kuridhiana kwa sababu hawakubaliani na Bakwata
ambalo kiongozi wake ni Mufti Mkuu wa Tanzania.
Walisema
maaskofu walisema hawana tatizo na suala la Mahakama ya Kadhi, lakini
isiwe na muundo kama wa mahakama nyingine na kwamba mawazo ya waasisi wa
Taifa, hawakutaka serikali iwe na dini na ndiyo maana hawakuruhusu
mahakama hiyo.
Mbunge
wa Viti Maalumu (CUF), Rukia Kassimu, alihoji ni kwanini Mahakama ya
Kadhi inataka kuundwa na kupewa jukumu Mufti ambaye anatoka Bakwata
ambayo ni taasisi binafsi na imesajiliwa na Mamlaka ya Rita.
“Bakwata
ni taasisi kama zilivyo taasisi nyingine, haikubaliki, Mheshimiwa
Waziri Mkuu aliahidi suala la Mahakama ya Kadhi ili Waislamu wampigie
kura kwa sababu anataka kugombea urais mwaka huu,” alisema.
Rukia
alisema ni marufuku serikali kuwalazimisha Waislamu kuwa chini ya
Bakwata na kwamba Waziri Mkuu, Pinda anafahamu kwa kina suluhisho na
mvutano huo wa Mahakama ya Kadhi.
Mbunge
wa Kasulu Mjini (NCCR), Moses Machali, alisema suala la kuanzishwa kwa
Mahakama ya Kadhi na kuingizwa katika mfumo wa mahakama za kawaida
inajichanganya na ibara ya 19 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Alisema
mwaka 2011 Rais Jakaya Kikwete wakati anazindua msikiti wa Gadaf
alisema suala la uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi lisihusishwe na
serikali kwa sababu wapo watu wengine ambao kila mmoja ana imani yake.
Alisema
hatua ya serikali kutaka kuuleta muswada huo wakati bado Waislamu
wenyewe hawaelewani ni kuwakosea Waislamu na kwamba inawezekana Waziri
alilizungumzia suala hili sababu ya malengo yake ya urais.
Machali
alisema kama muswada huu utapelekwa Bungeni itatoa fursa kwa madhehebu
mbalimbali kila moja kuanzisha mahakama yake hali itakayoleta machafuko
nchini kwa kuwa nchi itakuwa katika mfumo wa mahakama za dini.
Mbunge
wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alisema muswada
unapendekeza kutambua kitu ambacho mfumo wa sheria za nchi hauna na
kwamba uongo unaotumiwa na serikali ndiyo unafanya watu wawe na hofu.
Mbunge
wa Nkasi Kusini (CCM), Ally Kessy, alisema: “Katika nguzo tano za
Kiislamu Mahakama ya Kadhi haipo, nguzo sita za imani pia haipo, sasa
inakuwaje wanadai kitu ambacho hakitambuliki katika nguzo za kiislamu.”
Mbunge
wa Sumve (CCM), Richard Ndassa, alisema muswada wa Mahakama ya Kadhi
urudishwe ukaboreshwe badala ya kuharakisha kuupeleka bungeni wakati
bado una utata hata kwa waislamu wenyewe.
Mbunge
wa Tarime (CCM), Nyambali Nyangwine, alisema Muswada wa Mahakama ya
Kadhi usimamishwe ukafanyiwe utafiti kwanza kwa sababu ndani ya
Waislamu wenyewe hawaelewani.
Mbunge
wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini, alisema Wabunge wasipokuwa makini
na suala la Mahakama ya Kadhi, Bunge litaingia katika historia kuvunjika
kwa amani.
Selasini
alisema serikali iachane na kutoa ‘jini’ lililofungiwa na waasisi
Mwalimu Nyerere na Karume na kwamba tukifanya mchezo nchi itabaki katika
vipande vipande.
Mbunge
wa Viti Maalum (CCM), Dk. Mary Mwanjelwa, alisema jambo hili
litaligawa Taifa na kwamba waasisi hawakuwa wajinga walipokataa serikali
isiwe na dini.
Mbunge
wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa, alisema nchi inaelekea kubaya
kwani msingi wa kuleta Mahakama ya Kadhi ni kutaka kuwachota Waislamu
kwa ajili ya uchaguzi mkuu.
“Serikali
kama imedhamiria kuleta Mahakama ya Kadhi ilete katika utaratibu mzuri,
lakini kwa huu utaratibu ni unafiki na mwenyezi Mungu hapendi unafiki,
tusiwahadae Waislamu,” alisema.
Khalifa alisema kwa hali ilivyo muswada huo haujaiva na kwamba usiletwe bungeni hadi hapo serikali itakapojipanga vizuri.
Mbunge
wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde, alisema suala la imani
siyo la chama cha kisiasa kwani suala la Mahakama ya Kadhi litaipeleka
nchi kubaya na inawezekana ikawa ndio mwisho wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
“Mnataka
kutuvurugia nchi sababu ya kutafuta kura za Waislamu, kwa hili Waziri
Mkuu umechemka sana, nalisema hili kwa sababu wewe Waziri Mkuu ndiye
uliyeahidi kuleta bungeni Muswada wa Mahakama ya Kadhi,” alisema.
Mbunge wa Kisarawe (CCM), Suleiman Jafo, alisema yasifanyike masikhala mswaada huyo uwasilishwe bungeni.
Mbunge
wa Mbeya Vijijini (CCM), Mchungaji Lackison Mwanjale, alisema serikali
ikajipange upya katika suala la Mahakama ya Kadhi kabla ya kuuleta
bungeni muswada kwani bado suala hilo halieleweki kwa jamii.
Mbunge
wa Kilwa Kaskazini (CCM), Martaza Mangungu, alisema hakubaliani na
suala la Mufti kupewa jukumu la kuchagua Kadhi Mkuu wakati Waislamu
wengi hawakubaliani na Bakwata ambayo inaongozwa na Mufti.
Mbunge
wa Lupa (CCM), Victor Mwambalaswa, alisema muswada wa Mahakama ya Kadhi
wapelekewe wahusika kabla ya kuletwa bungeni ili wajadiliane na
kukubaliana mambo ya msingi wanayoona yatawafaa katika uanzishwaji wa
mahakama hayo.
Mbunge
wa Igunga (CCM), Dk. Peter Kafumu, alisema serikali imeshindwa
kusimamia vizuri suala la uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi kwa kushindwa
kuwaelimisha wananchi jambo hilo.
Mbunge
wa Chwaka (CCM), Yahaya Kassim Issa, alisema Waislamu wanataka
Mahakama hiyo kwa kuwa wanakosa haki hivyo serikali iruhusu kuanzishwa
kwake.
Pinda: Tutatafakari Upya
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, akihitimisha mjadala huo alisema kulingana na
maoni yaliyotolewa na Wabunge ameelewa kwamba bado hakuna maelewano
miongoni mwa Waislamu wenyewe na pia hakuna uelewa wa jamii kuhusu suala
hilo.
Alisema
mambo yaliyowasilishwa kuhusiana na muswada huo ni maamuzi ya Bunge
Maalum la Katiba na siyo yake, bali anabebeshwa msalaba tu kwa sababu
alikuwa anaiwakilisha serikali.
Pinda
alisema kutokana na hali hiyo, serikali itakaa kushauriana tena na
Spika pamoja na Rais waone wafanye nini katika jambo hilo.
Vijembe na Matusi
Mbunge
wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage, wakati akichangia hoja hiyo
alishindwa kuvumulia baada ya baadhi ya wabunge kuingilia mchango wake
kwa kumzomea na kusema maneno yaliyomuudhi na kuamua kuwatolewa maneno
ya kuudhi (matusi).
Mbunge
wa Fuoni (CCM), Said Mussa Zubeir, aliwaita baadhi ya wabunge walikuwa
wakimzomea wakati akizungumza kuwa ni ‘wapumbavu’.
Wakati
wa majadiliano hayo ilipofika saa 8:17 wakati Mbunge wa Kisarawe, Jafo
akiendelea kuchangia kulitokea vurugu ambazo nusura wabunge wapigane
huku baadhi yao wakiamua kutoka ukumbini.
Kutokana
na kutokuwapo hali ya utulivu ukumbini, baadhi ya askari pamoja na
maofisa usalama waliokuwapo nje, walilazimika kuingia ndani kuhakikisha
amani haivunjiki.
Spika wa Bunge, Anna Makinda, alituliza vurugu ukumbini kwa kuwataka wabunge wawe wavumilivu wakati wenzao wakichangia.
Katika
majadiliano wabunge zaidi 30 walichangia na zaidi ya 20 walikataa
muswada wa Mahakama ya Kadhi usiwasilishwe Bungeni siku ya Jumatano
wiki hii.
Kabla
ya kuanza majadiliano, Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia, alitoa hoja
kwa Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Katiba, Sheria na Utawala,
William Ngeleja, kwamba wakati wa majadiliano waandishi wa habari
wasiwepo ukumbini kwa kile alichoeleza ni unyeti wa jambo hilo.
Hata
hivyo, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Kessy, alisema kama waandishi
wataondolewa ukumbini naye atalazimika kuondoka huku Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, George Masaju, akisema hakuna sababu ya kuwaondoa waandishi
kwa sababu jambo linalojadiliwa wananchi wanataka kulifahamu kupitia
vyombo vya habari.
Masaju
akichangia wakati wa kujibu hoja za wabunge, alisema suala la mahakama
ya kadhi halina tatizo wala halivunji katiba kama ilivyoelezwa na baadhi
ya wabunge na kuwataka wabunge wamuheshimu wakati ana-zungumza.
إرسال تعليق