WASAFIRI RAIA WA CAMEROON WATEKWA NYARA

Wasafiri kadhaa raia wa Cameroon wameripotiwa kutekwa nyara na watu wasiojulikana karibu na mpaka wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Duru za kuaminika zimeripoti kuwa, watu hao 15 wametekwa nyara na watu wenye silaha wa kundi linaloongozwa na mtu mmoja anayetambulika kwa jina la Abdoulaye Miskine, huko kaskazini mashariki mwa Cameroon karibu na mpaka wa pamoja na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Chanzo kimoja cha usalama nchini Cameroon kimeeleza kuwa, wasafiri hao 15 walitekwa nyara usiku wa Alkhamis iliyopita katika kijiji cha Gbabio kilichoko umbali wa kilometa 10 kutoka mji wa Garoua-Boulaï, mashariki mwa Cameroon.
Chanzo hicho ambacho hakikutaka kutaja jina lake kimesema kuwa, bila shaka yoyote raia hao wa Cameroon walitekwa nyara na wanachama wa kundi la Abdoulaye Miskine ambalo ni maarufu kwa vitendo vya ukatili na machafuko mashariki mwa taifa hilo.
Kwa mujibu wa jeshi la polisi la Cameroon, wasafiri hao walitekwa nyara majira ya saa 11 za usiku kutoka katika mji wa Bertoua, makao makuu ya mkoa wa mashariki mwa nchi hiyo. Itakumbukwa kuwa mwaka uliopita, Abdoulaye Miskine alitiwa mbaroni karibu na mpaka wa Cameroon na Jamhuri ya Afrika ya Kati na kufungwa jela miezi kadhaa.
 CHANZO: BBC SWAHILI

Post a Comment

Previous Post Next Post