Kijana wa jamii ya wafugaji, Tiga Luchoma (15), ameuawa kwa kushambuliwa na wanyama wakali akiwa machungani.
Katika tukio lingine Flugence Sangana (22), mkazi wa kijiji Kiwurungi, wilayani Songea amejeruhiwa na Chui.
Akizungumza na NIPASHE jana, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa
Ruvuma, Revocatus Malimi, alilitaja tukio la kuuawa kwa Luchoma kuwa
lilitokea juzi majira ya saa 2 asubuhi katika kijiji cha Twendembile
ambako wakati akiwa machungani aliuawa kwa kutafunwa na wanyama wakali
ndani ya hifadhi ya Taifa ya Mbuga ya Selous.
Alisema kuwa masalia ya mwili wake yalikutwa kandokando ya mto Msisima ambako inahofiwa kuwa wanyama hao walimshambulia.
Alisema mpaka sasa wanyama waliomshambulia kijana huyo bado hawajafamika ni wa aina gani na uchunguzi unaendelea.
Alilitaja tukio jingine kuwa lilitokea juzi majira ya saa 2 asubuhi
huko katika kijiji cha Kiwurungi, ambapo Sangana alijeruhiwa vibaya na
chui dume sehemu mbalimbali za mwili wake.
Alisema Sangana alipatwa na mkasa huo wakati alipokuwa akilinda shamba la mazao lisishambuliwe na nyani.
Alisema kuwa hata hivyo, chui huyo aliuawa na wananchi waliofika
eneo la tukio baada ya kumsikia Sangana akipiga kelele ya kuomba msaada.
Majeruhi huyo amelazwa katika kituo cha afya cha Muhukuru kwa matibabu zaidi.
Malimi aliwataka wananchi wanoishi maeneo karibu na mbuga ya
wanyama, kutotembea mmoja mmoja ili kusaidiana wanyama wakali wanapotaka
kuwashambulia.
Post a Comment