Hali za majeruhi mashabiki wa Simba zaendelea vizuri.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo.
Hali za majeruhi wa ajali iliyohusisha basi dogo la abiria eneo la Makunganya, barabara kuu ya Morogoro-Dodoma lililokuwa na mashabiki wa timu ya Simba, zinaendelea vizuri, huku majeruhi mmoja akihamishiwa wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).
 
Aidha, miili ya watu watano kati ya saba  imeshatambuliwa, ukiwemo mwili wa Abdala Fundi, Abdala Uwadi, Nurdini Mayopa, Rehema Musa na Ramadhani Kingolini maarufu kama Ngumi Jiwe.
 
Mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk. Ritta Lyamuya, alisema ajali hiyo iliyotokea juzi usiku, walipokea majeruhi 23, ambapo wawili walifariki dunia wakipatiwa matibabu na watu watano waliopoteza maisha eneo la ajali.
 
Dk. Lyamuya alipongeza jitihada zilizofanywa na Mbunge wa Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood, kwa msaada wa vifaa tiba, mara tu baada ya ajali, jambo lililoongeza ufanisi wa utoaji wa huduma hospitalini hapo.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari hiyo kukosa umakini na kutokuwa na uzoefu wa barabara hiyo, ambayo imekuwa na utelezi katika eneo hilo mvua zinaponyesha, na kuwataka madereva kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani.
 
Abiria walionusurika katika ajali hiyo, walisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni utelezi uliosababishwa na mvua zilizokuwa zikiendelea kunyesha, uliomfanya dereva wa gari waliyokuwa wamepanda aina ya costa, yenye namba za usajili T 304 CWN kushindwa kumudu na kuserereka kwa umbali mrefu, kabla ya kupinduka na kukwama kwenye ukingo wa barabara.

Post a Comment

Previous Post Next Post