Hali za majeruhi wa ajali iliyohusisha basi dogo
la abiria eneo la Makunganya, barabara kuu ya Morogoro-Dodoma lililokuwa
na mashabiki wa timu ya Simba, zinaendelea vizuri, huku majeruhi mmoja
akihamishiwa wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).
Aidha, miili ya watu watano kati ya saba imeshatambuliwa, ukiwemo
mwili wa Abdala Fundi, Abdala Uwadi, Nurdini Mayopa, Rehema Musa na
Ramadhani Kingolini maarufu kama Ngumi Jiwe.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk.
Ritta Lyamuya, alisema ajali hiyo iliyotokea juzi usiku, walipokea
majeruhi 23, ambapo wawili walifariki dunia wakipatiwa matibabu na watu
watano waliopoteza maisha eneo la ajali.
Dk. Lyamuya alipongeza jitihada zilizofanywa na Mbunge wa Morogoro
Mjini, Abdulaziz Abood, kwa msaada wa vifaa tiba, mara tu baada ya
ajali, jambo lililoongeza ufanisi wa utoaji wa huduma hospitalini hapo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alisema chanzo
cha ajali hiyo ni dereva wa gari hiyo kukosa umakini na kutokuwa na
uzoefu wa barabara hiyo, ambayo imekuwa na utelezi katika eneo hilo mvua
zinaponyesha, na kuwataka madereva kuwa makini na kuzingatia sheria za
usalama barabarani.
Abiria walionusurika katika ajali hiyo, walisema kuwa chanzo cha
ajali hiyo ni utelezi uliosababishwa na mvua zilizokuwa zikiendelea
kunyesha, uliomfanya dereva wa gari waliyokuwa wamepanda aina ya costa,
yenye namba za usajili T 304 CWN kushindwa kumudu na kuserereka kwa
umbali mrefu, kabla ya kupinduka na kukwama kwenye ukingo wa barabara.
إرسال تعليق