Dar es Salaam. Tanzania inatarajia kuzindua
kituo cha kimataifa cha usuluhishi wa migogoro ya kibiashara kutokana na
kukua kwa sekta ya uwekezaji ikiwamo mafuta na gesi nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi
Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye alisema kituo hicho kitazinduliwa Juni
mwaka huu na kitasimamia na kutatua migogoro yote ya kibiashara
itakayojitokeza katika kipindi hiki cha ugunduzi wa gesi na mafuta.
Simbeye alisema, kuanzishwa kwa kituo hicho
kunatokana na kuongezeka kwa wawekezaji nchini, kuboresha biashara na
kuongezeka kwa wafanyabiashara wakubwa hasa baada ya kuzinduliwa kwa
sekta ya mafuta na gesi.
“Rwanda tayari imeanzisha kituo kama hicho,
kimesaidia kutatua migogoro ya kibiashara dhidi ya wawekezaji na
wafanyabiashara,” alisema.
Alisema hayo juzi, wakati akielezea maandalizi ya
mkutano wa kimataiafa wa usuhuhishi wa migogoro ya kibiashara
utakaofanyika jijini Dar es Salaam, Aprili 9 - 10 mwaka huu.
Simbeye alisema lengo la mkutano huo ni kujadili
namna ya kutatua migogoro ya kibiashara na kijamii nje ya mahakama bila
kufikishwa kwa kesi hizo mahakamani.
“Mkutano huu utashirikisha nchi za Afrika
Mashariki. Migogoro hiyo itatatuliwa bila kesi kufikishwa mahakamani
kwa sababu tunaona mashauri mengi yanatumia muda mrefu kutolewa hukumu
lakini tukishiriana na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) na TPSF
tunaweza kutatua migogoro hiyo nje ya mahakama,” alisema Simbeye.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wanasheria wa
Tanganyika (TLS), Kaleb Gamaya alisema kupitia mkutano huo, washiriki
watapata nafasi ya kuangalia jinsi ya kutatua migogoro nje ya utaratibu
wa mahakama kama nchi zilizoendelea zinavyofanya.
“Usuluhishi wa migogoro unaofanyika mahakamani
unaweza kumalizika baada ya miaka mitatu, hivyo kibiashara unakuwa
umeathiri uchumi kwa sababu ya muda wa kupitia mashauri, ndiyo maana
tukaona kuna haja ya kujitosa kuanzisha utaratibu huu,” alisema Gamaya.
Aliongeza: “Lengo la TLS ni kujadili na kushawishi
wanachama wetu kuwapo katika mkutano huu na washiriki watapata elimu
na faida ya usuluhishi nje ya mahakama,” alisema.
Alisema mkutano huo wa tatu kufanyika Afrika,
utajadili migogoro ya mafuta na gesi kwa sababu ni kitu kipya nchini na
kwamba mikutano kama hiyo ilishawahi kufanyika Nairobi na Addis Ababa
miaka mitatu iliyopita.
Mratibu wa mkutano huo kutoka Mtandao wa
kibiashara wa Afrika Mashariki, Martha Yeronimo alisema watu zaidi ya
200 wanatarajia kushiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania
إرسال تعليق